TIMU ya Taifa ya netiboli ya Tanzania ‘Taifa Queens’ imeweka hai matumaini ya kupata medali katika mashindano ya All Africa Games yanayoendelea jijini Maputo, Msumbiji.
Habari zilizopatikana kutoka Maputo, zilieleza kuwa hatua hiyo inatokana na ushindi wa magoli 32-29 ilioupata jana dhidi ya Afrika Kusini. Ushindi huo umerudisha matumaini baada ya juzi timu hiyo kufungwa na Uganda magoli 52-41.
Uganda tayari imejihakikishia kutwaa medali ya dhahabu, ambapo ndiyo timu pekee ambayo haijafungwa mchezo tangu mashindano hayo yaanze yakihusisha timu tisa zinazocheza mfumo wa ligi.
Taifa Queen imecheza michezo saba, imeshinda mitano na kupoteza miwili, ambapo leo itamaliza michuano hiyo kwa kucheza na Botswana. Botswana na Zambia nazo zina nafasi kubwa ya kutwaa medali kama zitashinda mechi zao za leo.
Mwaka 2007 katika mashindano kama hayo yaliyofanyika Algiers, Algeria, Tanzania ilipata medali moja ya fedha iliyonyakuliwa na Martine Sulle katika mbio za nusu Marathon.
Habarileo.co.tz



0 comments