Saturday, September 24, 2011

Waliokosa mikopo waingiwa na mashaka ya kupoteza nafasi za masomo

WANAFUNZI waliokosa mikopo kwa elimu ya juu, wameiomba serikali kulipatia ufumbuzi tatizo lao kwa kuwa muda wa kuripoti vyuoni unazidi kukaribia, huku wakielezea hofu yao kwamba huenda wakazipoteza nafasi za kusoma vyuo vya elimu ya juu nchini kutokana na kutokuwa na fedha.

Mwenyekiti wa wanafunzi waliokosa mikopo kwa mwaka 2011/12, Samwel Nshatsi, alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Wanaomba Serikali ichukulie uzito suala hili na iwapatie ufumbuzi mapema kwa sababu siku zao za kuanza masomo zinazidi kusogea na kwamba wanahofia nafasi zao kwenda chuo kupotea.

Nshatsi alisema, kwa mujibu wa majina yaliyotolewa na bodi ya mikopo nchini, ni zaidi ya 14,000 ya wanafunzi waliokosa mikopo.

Alisema kuwa, awali Septema 5, mwaka huu walifanya kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Mafunzo ya Ufundi, Mkurugenzi wa Elimu ya juu na Kamishna wa Elimu ya juu na baadhi ya watendaji wa bodi ya mikopo, na wakawasilisha malalamiko yao.

Waliahidiwa kupewa majibu rasmi Septemba 12, mwaka huu, lakini haikutekelezwa, wakaahidiwa kupatiwa Septemba 20.

Alisema, Septemba 13, wakaamua kumwandikia barua ya maombi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa. Hata hivyo Septemba 20, badala ya kupatiwa majibu waliyotarajia, wakaitwa kwenye kikao kingine na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya juu, wakaelezwa kuwa isingewezekana kupatiwa majibu siku hiyo.

Kadhalika, Katibu alikiri kupokea waraka ulioandikwa na alidai aliliona suala la kundi hili kuwa hatarini kupoteza nafasi zao vyuoni na akamuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya juu kulifanyia kazi.


habarileo.co.tz

No comments:

Post a Comment