Monday, September 26, 2011

WAMA kujenga viwanja vya michezo

MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake Nchini (WAMA) ambaye pia ni mke wa Rais, Salma Kikwete, amesema kuwa taasisi yake imepanga kujenga viwanja vya michezo katika Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama iliyoko katika kijiji cha Nyamisati, Kibiti Rufiji, mkoani Pwani.

Salma Kikwete aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohammed Shein, ambapo kulikuwa na hafla ya uzinduzi wa shule hiyo yenye wanafunzi 510.

“Kwa kuwa michezo ni afya tutajenga viwanja vya soka, netiboli, mpira wa kikapu, tenisi na mingineyo,” alisema.

Wakati huohuo Mbunge wa Viti Maalum, Vicky Kamata, juzi alimwagiwa sifa na Waziri wa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, kutokana na umahiri wake wa kutunga wimbo wenye maudhui husika kuhusu mtoto wa kike.

“Napenda kusema kweli Vicky wewe unastahili sifa katika kutunga wimbo huu kwani umetutoa machozi sisi wengine; hongera sana na ahsante kwa kutuburudisha pia,” alisema Ghasia.

Vicky aliyetunga na kuimba wimbo huo mahsusi kwa kutoa pongezi kwa Salma Kikwete katika hafla hiyo; aliimba na kucheza na wanafunzi wa shule hiyo.

Wimbo huo ulikuwa ukizungumzia kuwatia moyo watoto wa kike wa shuleni hapo ambao miongoni mwao ni yatima na wanaoishi katika mazingira magumu waliopata ufadhili kutoka sehemu mbalimbali nchini.



Tanzania daima

No comments:

Post a Comment