DHANA ya kujivua gamba iliyoasisiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, na ambayo hivi karibuni ilimng’oa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, imeingia katika hatua ngumu ya utekelezaji wake, Tanzania Daima Jumatano, limebaini.
Ugumu wa hatua ya sasa unatajwa na wafuatiliaji wa siasa za ndani za CCM kuwa unasababishwa na mwelekeo wa dhana hiyo kuonekana ukielekea kumlenga Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Kuibuka upya kwa siasa zenye mwelekeo wa uhasama mkali kati ya kundi moja la viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa chama hicho, Nape Nnauye, kunaelezwa kuwa ni matokeo ya mwelekeo wa sasa wa dhana hiyo.
Viongozi hao wa vijana wanaoongozwa na Kaimu Mwenyekiti wao wa Taifa, Benno Malisa, anayeungwa mkono na Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Arusha, James Millya, wanatajwa kuwa watu ambao wamekuwa wakipinga harakati zinazopigiwa chapuo na Nape za kuendelea kwa utekelezaji wa dhana hiyo ya kujivua gamba.
Wakati Nape na wana CCM wengine wenye msimamo kama wake wakiitaja hatua ya Benno, Millya na vijana wenzao wa Arusha kuwa inayolenga kukwamisha utekelezaji wa dhana hiyo, kundi hilo linalompinga linamtuhumu kwa kukivuruga chama chao kwa maslahi yake binafsi.
Sakata hili jipya liliibuka baada ya Benno kuliongoza kundi kubwa la vijana wa chama hicho kufanya maandamano katika jiji la Arusha hivi karibuni yaliyomalizika kwa kauli nzito kutoka kwao ambao mbali ya kuelekezwa kwa Nape zilimtuhumu pasipo kumtaja kwa jina mtoto mmoja wa kigogo kuwa alikuwa nyuma ya mpango wa kuwazuia kutekeleza ajenda yao.
Hatua hiyo ya Benno ambayo baadhi ya wadadisi wa mambo wanaifananisha kuwa ni kubadili mwelekeo wa mapambano ya kisiasa inamweka mwanasiasa huyo kijana katika kundi la watu wanaopinga hatua zozote za kujaribu kumng’oa Lowassa katika uongozi wa chama hicho.
Wadadisi hao wa mambo wanaielezea hatua hiyo ya Benno na wenzake kuwa inalenga kumuonyesha Kikwete na CCM kutounga mkono hatua ya namna yoyote ya kumuwajibisha Lowassa na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, wakati wa kikao kijacho cha NEC kinachotarajiwa kukutana Novemba, mwaka huu.
Wakihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la wazi karibu na hospitali ya Mt. Thomas, Benno na Millya, walisema kitendo cha mtoto mmoja wa kiongozi wa juu wa chama kuamuru polisi kuwakamata na kuzuia ziara yao ya ufunguaji wa mashina ni cha kinyama na matumizi mabaya ya madaraka.
Ingawa hawakumtaja kwa jina, ni wazi kwamba viongozi hao walikuwa wakimlenga mmoja wa watoto wa viongozi wa juu wa CCM na serikali (jina tunalo) ambaye amekuwa mstari wa mbele katika harakati za siasa za mzazi wake kwa muda mrefu sasa.
“Inasikitisha kuona kwamba zinapigwa simu nyingi ili tunyimwe nafasi ya kufanya mkutano na kufungua matawi. Huu si mkutano wa kampeni wa kutafuta urais, wala hatumnadi mgombea wa urais, sasa ujinga huu unatoka wapi?” alisema Benno.
Hata hivyo, mwanasiasa huyo kijana hakuweza kusoma hotuba yake aliyoiandaa na badala yake akaishia katika kuwashambulia Nape na mtoto huyo wa kigogo.
Wakati Nape akishangilia ushindi wa chama chake kilioupata Igunga, kwa kutoa kauli kuwa “kujivua gamba kumelipa” na “Tanzania ina wenyewe na wenyewe ni CCM”, Benno katika hotuba yake hiyo ya Arusha alimpinga akisema, “Ni aibu kwa kiongozi kudai eti Tanzania ni ya CCM wakati anajua kuwa ni ya watu wote wanaotakiwa kushirikiana kwa umoja na mshikamano kujenga taifa lao.”
Siku moja baada ya Benno na vijana wenzake wa Arusha kurusha makombora hayo, Nape aliibuka na akasisitiza azma ya chama hicho kuendelea na harakati zake za kutekeleza dhana ya kujivua gamba.
Mbali ya Nape kuwajibu kina Benno, alitumia fursa hiyo kushambulia kundi moja la wanasiasa ndani ya CCM akisema limeandaa hujuma dhidi ya Rais Kikwete kwa kupanga kumvua uenyekiti wa chama hicho na kumbakizia urais.
Pasipo kumtaja yeyote kwa jina, Nape alisema kundi hilo kuwa ndilo lile lile ambalo siku zote limekuwa nyuma ya ajenda ya kupinga maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ya kupinga dhana ya kujivua gamba.
Mbali ya kuzungumza hayo wiki iliyopita, Nape ameibuka tena Mwanza Mjini majuzi, juzi na jana akiendelea kutoa matamshi makali dhidi ya wale anaowaita mafisadi na makundi yao.
Akizungumza kwa kujiamini katika moja ya mikutano yake jana, Nape amekaririwa akisema, watuhumiwa wa ufisadi na makundi yao watakuwa wakijidanganya na kufanya makosa iwapo wanadhani wanaweza kukifanya CCM kuwa kichaka cha kujificha.
Nape ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya Igoma, Sokoni alitumia mifano kadhaa katika vitabu vitakatifu kujenga hoja zake.
Akitoa mfano alisema, harakati za CCM kujisafisha kwa kuwaondoa waovu ni sawa na kile alichofanya Bwana Yesu Kristo wakati alipopindua meza za wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara ndani ya sinagogi.
Alieleza kushangazwa na baadhi ya viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kujilimbikizia mali na ambao wanapowajibika serikalini wanaenda kujificha kwenye chama.
Wakati mzozo kati ya Nape na vijana wa UVCCM ukiendelea, taarifa ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata kutoka Arusha zinaeleza kuwa, Lowassa amefikia hatua ya kuitisha mkutano wa waandishi wa habari huko Monduli leo hii.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata kutoka Monduli zinaeleza kuwa mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akijitokeza mara chache katika vyombo vya habari ameitisha kikao hicho akionyesha kukerwa na hatua ya kuhusishwa karibu na kila jambo baya linalotokea ndani ya CCM.
Taarifa hizo zinasema katika mkutano wake huo, Lowassa atautumia kukanusha tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake zikiwemo ya kuhusishwa kwake na matukio yanayowahusu vijana hao wa UVCCM na mipango mingine ya kukihujumu chama chake.
Mtoa habari wetu aliyezungumza na gazeti hili amesema, Lowassa anatarajia kujibu baadhi ya hoja ambazo zina mwelekeo wa kumgusa yeye ambazo zimekuwa zikitolewa na Nape na wanasiasa wengine ndani ya CCM.
tanzanai daima
0 comments