BONDIA wa ngumi za kulipwa hapa nchini, Japhet Kaseba ameibuka bingwa wa Taifa wa uzani wa Kati kg 72 baada ya kumkung'uta mpinzani wake Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo' kwa pointi 100-91 katika pambano lililofanyika juzi Usiku kwenye ukumbi wa Travertaine, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Ilikuwa vigumu kutabiri nani ataibuka bingwa katika pambano hilo lililokuwa la raundi kumi lililosimamiwa na Organizesheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania 'PST' ambapo Mtambo wa Gongo alionekana kuhimili mikiki ya Kaseba katika raundi zote za pambano.
Hata hivyo mashabiki waliokuwa wamefurika ukumbini hapo kabla ya kuanza kwa pambano hilo walionekana kumtabiria ushindi Mtambo wa Gongo kutokana na rekodi yake nzuri katika masumbwi Afrika Mashariki huku wakionekana kuwa na wasiwasi na Kaseba ambaye ana rekodi ya kukung'utwa na mahasimu wake Francis 'SMG' Cheka na Mada Maugo.
Hata hivyo utabiri huo uligeuka shubiri kwa mtambo wa Gongo katika raundi ya tano ya pambano baada ya kukubali makonde mfululizo ambapo hadi dakika tatu za raundi hiyo zinamalizika mashabiki wa bondia huyo nguli miaka ya nyuma walikuwa kimya huku wale wa Kaseba wakionekana kulipuka kwa furaha.
Raundi ya kwanza hadi ya nne ya pambano hilo mchezo ulikuwa wa piga nikupige huku kila mmoja akijaribu kurusha makonde ya malengo ambayo yalionekana kuzaa matunda kwa pande zote mbili katika raundi hizo.
Raundi ya sita Mtambo wa Gongo alizinduka na kurusha makonde ya uhakika kwa mpinzani wake wakati raundi ya saba, nane na tisa mabondia hao walitupiana makonde kwa zamu hali iliyokwenda hadi raundi ya kumi na ya mwisho wa mchezo na Kaseba kuibuka kinara kwa pointi 100-91.
Baada ya ushindi huo Kaseba alisema kuwa, "Ilikuwa vigumu kutwaa ubingwa huu, mpinzani wangu alicheza vizuri huku akionekana alikuwa amejipanga kikamilifu kwa ajili ya ushindi hata mashabiki walitarajia hilo. "Lakini nashukuru nimefanikiwa na sasa mimi ndiyo bingwa wa taifa wa uzani wa kati, ila ninachotaka kusema kwa mashabiki wangu ni kwamba ndiyo nimerejea katika masumbwi na huu ni mwanzo tu," alisema Kaseba.
Hata hivyo mtambo wa Gongo alikubaliana na matokeo hayo na kudai kuwa katika mchezo lazima kuna kushinda na kushindwa licha ya kuwa amecheza vizuri, lakini mpinzani wake alimzidi mbinu za kimchezo.
Kaseba aliwai kutangaza kuachana na ngumi na kugeukia katika mchezo wa ngumi na mateke 'kick boxing' baada ya kukung'utwa na Cheka, aliamua kurejea tena katika masumbwi ambapo alicheza na Maugo na kupigwa kwa pointi na kujiondoa katika mchezo huo kwa mara nyingine tena kabla ya juzi kutangaza kurejea upya katika masumbwi.
mwananchi.co.tz
0 comments