MWANAFUNZI wa Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mwapachu iliyoko Kata ya Tangasisi jijini Tanga amekufa baada ya kujinyonga usiku kwa kutumia kamba ya manila.
Mwanafunzi huyo ambaye alikuwa yatima, amefahamika kwa jina la Sudi Omari (19) mkazi wa Mwakidila ‘A’ na kabla ya kujinyonga juzi alikuwa tayari amefanya mitihani mitano ya kumaliza kidato cha nne iliyojumuisha masomo ya Hisabati, Uraia, Jografia, Kiswahili na Baiolojia. Mitihani ya kidato cha nne inatarajiwa kumalizika Oktoba 22 mwaka huu.
Ofisa Upelelezi Mkoa wa Tanga, Jaffari Mohammed akithibitisha tukio hilo ofisini kwake jana na kusema tukio hilo lilitokea Oktoba 6, mwaka huu baada ya mama yake mlezi wa Sudi kuingia chumbani saa 12.30 asubuhi na kukuta akiwa amejitundika darini.
“Ni kweli tumepokea taarifa ya kujinyonga kwa mwanafunzi aliyekuwa akisoma kidato cha nne katika Sekondari ya Mwapachu na alitumia kamba ya maila chumbani anakolala ila mpaka sasa bado hatujapata chanzo uchunguzi unaendelea,” alisema.
Kwa upande wake Ofisa Elimu ya Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, Kassim Sengasu akizungumza katika mahojiano na HABARILEO alisema tukio hilo limemsikitisha sana hasa kwa kupoteza kijana ambaye darasani alikuwa na uwezo mkubwa.
“Juzi (jana) mchana nilipokea taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Mwapachu aitwaye Cornel Rambau akinijulisha kuwa Sudi hakufika kwenye mtihani wa somo la Historia uliofanyika siku ya Jumatano mchana kwakuwa amefariki baada ya kujinyonga na hivyo yeye anakwenda kutazama maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo na nikaamua kuambatana naye,” alieleza.
Sengasu alibainisha kuwa Sudi ambaye ni yatima tangu alipokuwa darasa la kwanza alikuwa akiishi na mama yake mdogo, Manahuru Athuman huko Mwakidila, lakini alikuwa akipata msaada kutoka kwenye taasisi isiyo ya kiserikali ya kusaidia yatima iitwayo AFRIWAG yenye makazi yake jijini hapa.
Ofisa Elimu huyo aliongeza kuwa pamoja na kuwa yatima Sudi ni miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakifanya vizuri darasani na kwamba shuleni hapo alikuwa miongoni mwa wanafunzi wachache wanaotarajiwa kufaulu mtihani huo kwa kupata daraja la kwanza au la pili.
Naye Mwanahuru aliyekuwa mlezi wa kijana huyo, alisema hadi majira ya usiku walishiriki chakula cha usiku pamoja na kila mmoja aliendelea na shughuli zake, majira ya saa kumi usiku walisikia kelele za baiskeli kama ikigongwa wakahisi kuwa labda ni mwizi.
Mwanahuru alisema baada ya hali hiyo kuendelea kwa muda jirani yao alianza kumwita marehemu, lakini kimya kilitawala hali iliyowaingiza hofu ambapo waliamua kwenda chumbani kwa marehemu na kumkuta akining’nia huku anatoa sauti ya kukoroma.
Sudi alizikwa jana mchana baada ya sala ya Ijumaa kwenye makaburi yaliyoko eneo la Mapinduzi katika Kata ya Tangasisi katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Habarileo.co.tz
0 comments