MAMLAKA ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, imeziruhusu meli ya Mv Serengeti ambayo ilizuiwa kutokana na ubovu wa mashine mara kwa mara na Mv Sepideh iliyokuwa ikifanyiwa matengenezo kwa muda mrefu, baada kuridhika na ukaguzi iliofanya.
Akizungumza ofisini kwake Malindi mjini hapa, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Haji Vuai Ussi, alisema meli hizo zimekamilisha taratibu zote za mamlaka walizotakiwa.
Hata hivyo, Ussi alisema ruhusa hiyo imefuatia baada ya mamlaka kuridhika na ukaguzi uliofanywa na mkaguzi wa Serikali Septemba 28 na kugundua kuwa vyombo hivyo vinaweza kuendelea na ratiba zake.
“Mamlaka imeridhishwa na viwango vya vyombo hivi, ndiyo maana vimeruhusiwa,” alisema Ussi.
Alisema kuanzia leo meli hizo zitaanza safari zake kama kawaida, Serengeti itakwenda Unguja na Pemba na Sepideh itaendelea na safari zake za Dar es Salaam, Unguja na Pemba.
Akitaja sababu za kuzuiwa kwa vyombo hivyo, Ussi alisema ilitokana na hitilafu za ufundi kwenye mashine, jambo ambalo lilikuwa likitishia usalama wa abiria.
Pia, aliomba wananchi wa Zanzibar na Dar es Salaam kutumia meli hizo, kwani hivi sasa ni salama na kuwataka waondokane na hofu zilizojengeka mioyoni mwao.
“Wananchi wamekuwa na hofu kutokana na ajali zinazokumba meli hizi, lakini hii mamlaka inasema ziko katika kiwango kinachotakiwa,” alisema.
Wiki iliyopita, mamlaka hiyo ilifungia meli tano kutokana na ubovu na kwamba, zingine zilikuwa hazijakamilika taratibu za kubeba abiria, kwa sababu zilikuwa zimesajiliwa kwa ajili ya kuvuta meli mbovu baharini.
Septemba 10, mwaka huu meli ya Mv Spice Islander ilizama eneo la Nungwi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200, huku wengine zaidi ya 600 wakiokolewa. Hata hivyo, idadi ya waliokufa ni zaidi kutokana na wengine hawajaonekana hadi sasa na meli hiyo haijaibuliwa kutoka baharini.
mwananchi.co.tz
0 comments