Saturday, October 15, 2011

Zawadi za washindi wa mbio za beiskeli Mwanza zatajwa

WAANDAAJI na wadhamini wa mbio za baiskeli zijulikanazo kama “Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge” wametangaza zawadi zitakazotolewa kwa washindi mbalimbali watakaoshiriki mashindano ya mbio hizo zitakazofanyika kuanzia Shinyanga mjini mpaka jijini Mwanza Oktoba 23, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, juzi katika makao makuu ya Vodacom Tanzania yaliyoko Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Rukia Mtingwa, alisema kwamba kampuni yake imetenga zaidi ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo.

Alisema mwaka huu wameboresha mashindano hayo katika kila idara ambapo washiriki watashindana katika mbio za kilomita 150 kwa wanaume, 80 kwa wanawake, huku kwa upande wa walemavu watashindana katika kilometa 15 kwa walemavu wanaume na kilomita 10 kwa walemavu wanawake.

Mtingwa alisema mshindi wa kilometa 150 atajipatia shilingi 1,500,000, wa pili shilingi 1,000,000, wa tatu shilingi 700,000, mshindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja ataondoka na shilingi 500,000, mshindi wa 11 hadi 20 kila mmoja atajinyakulia shilingi 250,000 na mshindi wa 21 hadi 30 atapata shilingi 150,000 kila mmoja.

“Kwa upande wa mbio za mita 80 kwa wanawake mshindi wa kwanza atajipatia shilingi 1,100,000, wa pili shilingi 800,000, mshindi wa tatu atapata shilingi 600,000, wakati washindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja atazawadiwa shilingi 350,000, mshindi wa 11 hadi 20 kila mmoja atazawadiwa shilingi 130,000 na mshindi wa 21 hadi 30 watapatia shilingi 100,000 kila mmoja,” alisema.

Kwa upande wa mbio za kilometa 15 ambazo zitawashirikisha watu wenye ulemavu, washindi wa kwanza wawili kila mmoja atajipatia jumla ya shilingi 500,000, washindi wa pili wawili nao watajishindia shilingi 250,000 kila mmoja, washindi wa tatu wawili kila mmoja atapewa shilingi 150,000 kila mmoja wakati washindi wa nne wanne hadi wa kumi watajipatia shilingi 100,000 kila mmoja na watakaoshika nafasi ya 11 hadi ya 20 kila mmoja atazawadiwa shilingi 70,000.

Aidha Mtingwa alisema katika kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Vodacom itatoa zawadi maalumu kwa mshiriki atakayekuwa na umri wa miaka 50 kwenda mbele ambaye atamaliza mbio hizo ndani ya washiriki 50 wa kwanza kwa upande wa wanaume atajipatia shilingi 300,000 na kwa upande wa wanawake ataondoka na shilingi 300,000.



Tanzania Daima

0 comments