Tuesday, October 18, 2011

Zitto, January wamkalia kooni Ngeleja

WENYEVITI wa Kamati za Bunge za Nishati na Madini, January Makamba na Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe wamesema ikiwa hali ya umeme itaendelea kuwa mbaya nchini, itamlazimu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kujiuzulu.Kadhalika, wenyeviti hao wamesema hakutakuwa na uhalali wa Serikali kuzilipa kampuni zilizopewa jukumu la kuzalisha umeme wa dharura ikiwa umeme huo hautapatikana katika muda uliotarajiwa.

Wakizungumza Dar es Salaam juzi usiku kwenye mdahalo kuhusu ‘Hali ya Umeme nchini na Tanzania tunayoitaka’ ulioandaliwa na Kampuni ya Vox Media, wabunge hao waliuponda mpango wa dharura wa Serikali wa kukabiliana na mgawo wa umeme wakisema hautekelezeki.Katika mdahalo huo uliorushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Star, January alisema: “Bora kutokuwa Waziri kuliko kuwa waziri ambaye kauli zake haziaminiki kwa umma.”

Alisema kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake za kuondoa mgawo wa umeme, lazima waziri husika awajibike kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika nchi za magharibi.

Hata hivyo, January ambaye ni pia Mbunge wa Bumbuli (CCM) na Katibu wa Mambo ya Nje na Siasa wa CCM, alisema suala la kujiuzulu kwa waziri linategemea zaidi uadilifu wake na mamlaka iliyomteua kushika wadhifa huo.

Kwa upande wake, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) alisema: “Niliwahi kusema bungeni kwamba kila waziri aandike barua ya kujiuzulu ‘in advance’ (mapema) ili pale anaposhindwa kutekeleza wajibu wake, kazi ya Spika inakuwa ni kuchukua ile barua na kumkabidhi Rais.”

Alisema katika hali ya sasa, Serikali imeshindwa kutimiza ahadi iliyoitoa bungeni kuhusu utekelezaji wa mpango wa dharura wa kuzalisha umeme ili kuwezesha nchi kuondokana na mgawo na kwamba hilo tu linatosha kumfanya waziri ajiuzulu wadhifa wake.

Mpango wa dharura Wabunge hao walisema kuna kila dalili kwamba huenda mpango wa dharura wa kukabiliana na giza nchini ambao uliwasilishwa na Serikali bungeni usitekelezeke.

Mpango huo ni ule uliowasilishwa bungeni na Waziri Ngeleja Agosti 13, mwaka huu akiliomba Bunge liidhinishe kiasi cha Sh523 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wake. Mpango huo unaonyesha kuwa kutokana na dharura hiyo, Tanesco lilitarajiwa kukusanya kiasi cha Sh115 bilioni kutoka kwa wateja wake, hivyo kubakisha pengo la Sh408 bilioni ambazo Serikali iliahidi kwamba ingezitafuta katika vyanzo vingine.

Zitto alisema kutokana na hali hiyo, wabunge wanatarajia kuhoji katika Mkutano wa Tano wa Bunge la 10 unaotarajiwa kuanza Novemba 8, mwaka huu mjini Dodoma na kuitaka Serikali iwe na majibu.

“Kuna masuala ya ‘procurement’ (ununuzi), sheria lazima ifuatwe sasa ukiangalia mfano watu wa NSSF (Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii) ambalo linatakiwa kuzalisha megawati 150, hadi sasa bado hawajaanza kuingiza umeme kwenye gridi ya taifa, lakini Serikali ilileta mpango wake na wakasema wana uwezo wa kuutekeleza, kazi yetu ni kusubiri majibu,” alisema Zitto.

Alisema katika mchakato wa kutafuta mashine za kuzalisha umeme, NSSF lilinusurika kutapeliwa pale wataalamu wake walipofika Marekani na kubaini kwamba mtu waliyekuwa wakiwasiliana naye kwa ajili ya kupata mtambo huo, hakuwa na mashine wala kampuni ya aina hiyo.

Kauli hiyo iliungwa mkono na January aliyesema: “Kwanza ukiangalia mpango wenyewe wa dharura, vyanzo vyote ni vya mafuta au mafuta mazito ya dizeli au ya ndege. Huu umeme ni ‘very expensive’ (ghali mno), kwa nchi ambayo ni tajiri wa makaa ya mawe, gesi asilia na rasilimali nyingine.

Ni ‘scandal’ (kashfa) kutumia umeme huu,” alisema January na kuongeza: “Nasema ni ‘scandal’ (kashfa) kwa sababu kitaalamu umeme unaotokana na makaa ya mawe gharama yake ni senti 10 hadi 12 za Marekani kwa megawati moja, gesi ni kati ya senti za 8 hadi 12 za Marekani wakati umeme wa mafuta ni senti kama 42 za Marekani, sasa mtaona jinsi tunavyopoteza fedha nyingi kwa sababu zisizo za msingi.”

Alisema ukodishaji wa mitambo ya umeme wa dharura inayotumia mafuta ni mzigo kwa walipa kodi ambao ni maskini na kwamba fedha zinazotumika zingeweza kugharamia shughuli nyingine za maendeleo.

Alisema kwa taarifa alizonazo, kampuni ambazo tayari zimeingiza umeme wa dharura ni Symbion (megawati 37), IPTL (megawati 80) na Agrreko (megawati 50) na kwamba kiasi hicho cha umeme hakifikii nusu ya kile kilichoahidiwa na Serikali bungeni ambazo ni megawati 572 hadi Desemba mwaka huu.

Mbunge huyo alisema ikiwa umeme huo wa dharura hautapatikana wote ifikapo Desemba, basi hakutakuwa na maana ya dharura na kwamba hapo Serikali itabidi ipitie upya suala la malipo kwa kampuni husika.

“Dharura maana yake ni kutupatia umeme ‘within’ (kati ya) sasa na Desemba, sasa kama hadi leo NSSF hawajaweza kutupa zile megawati 50 tulizoahidiwa kwamba zitakuwa tayari Septemba na tunawadai na hizi nyingine za Oktoba, sidhani kama wanaweza kutimiza ahadi hiyo, hivyo lazima hili tuliangalie na hii ni kazi yetu sisi wabunge,” alisema January.

Chini ya mpango wa dharura, NSSF wanatarajiwa kuingiza katika gridi ya taifa megawati 150 za umeme, Symbion megawati 205, Agrreko megawati 100 na IPTL megawati 80 ambazo tayari zimeingizwa baada ya kupatikana kwa mafuta mazito.

Vyanzo mbadala Kutokana na athari za mgawo wa umeme, wabunge hao waliitaka Serikali kuchukua hatua za kutekeleza ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wabunge na wataalamu wa nishati.

Katika matamshi yao, wabunge hao kutoka kambi mbili tofauti bungeni, walikubaliana kwamba kimsingi suala la matumizi ya gesi na makaa ya mawe ndiyo suluhisho la matatizo ya nishati ya umeme nchini lakini wakaiponda Tanesco kwamba haina uwezo wa kusimamia sekta hiyo peke yake.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaalamu, miradi ya makaa ya mawe ya Ngaka mkoani Ruvuma, Kiwira mkoani Mbeya na Mchuchuma mkoani Iringa, ina uwezo wa kuzalisha megawati 1,500 za umeme kwa miaka 150, hivyo kulisaidia taifa kuondokana na giza.

Zitto alisema suala la Tanesco kufanyiwa marekebisho kwa maslahi ya Taifa halina mjadala ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi tofauti na sasa ambako limeshindwa kukidhi matakwa ya umma.

“Shirika hili linaweza kugawanywa sehemu mbili, kukawa na uzalishaji peke yake na sehemu ya usafirishaji na usambazaji nazo zikawa peke yake maana hivi sasa haliwezi kufanya kazi yake ipasavyo,” alisema Zitto.

Hata hivyo Naibu Kiongozi huyo wa upinzani Bungeni na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, aliwalaumu wanasiasa kwa kuingilia utendaji wa Tanesco na kwamba matatizo mengi ya shirika hilo la umma, yamechangiwa na kutolewa kwa maelekezo ya kisiasa yanayopingana na utaalamu.
“Lazima sasa kila mtu atekeleze wajibu wake, Tanesco tuwaachie wataalamu, Serikali ibaki na masuala ya kisera na sisi wabunge tubaki na ‘role’ (nafasi) ya usimamizi, hapo tutasonga mbele,” alisisitiza Zitto.

Katika maoni yake, January alisema Tanesco haiwezi kumudu kusimamia miradi mikubwa ya umeme na kwamba ipo haja ya kugawanywa katika sehemu tatu kwa maana ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuongeza ufanisi wake.

Alisema kugawanywa kwa shirika hilo kutapunguza upotevu wa umeme ambao kwa takwimu za mwaka jana, ulipotea kwa asilimia 25, kiwango ambacho ni sawa na umeme wote uliotumiwa viwandani au asilimia 75 ya umeme wote unaozalishwa na kampuni ya Songas.

“Kuna matatizo mengi sana ambayo yanapaswa kutatuliwa, kwani upotevu wa umeme mwingi kwa kiasi hiki na ni hatari sana, nadhani marekebisho yatakayofanywa yanaweza kusaidia kuondoa matatizo hayo,” alisema.

Ngeleja, Tanesco Katika mdahalo wa juzi, viongozi wa Serikali waliingia mitini kwa maelezo kwamba Waziri pamoja na watendaji wote wa sekta ya umeme katika Wizara ya Nishati na Madini wako safarini.

Mwenyekiti wa Mdahalo huo, Rosemary Mwakitwange alisema, Waziri Ngeleja alikuwa amealikwa na kwamba kulikuwa na ahadi kwamba lazima Serikali ingewakilishwa lakini akashangazwa na kutoshiriki kwao katika tukio hilo.
Kwa upande wake, Tanesco liliwakilishwa na Mkurugenzi wake wa Uwekezaji, Katyega Maneno ambaye alipata wakati mgumu pale alipotakiwa kujibu hoja za washiriki wa mdahalo huo.

Katyega alisema Tanesco linafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa umeme wote wa dharura unaanza kuzalishwa kabla ya Desemba mwaka huu kama Serikali ilivyoahidi.

“Tumeshajiandaa hata kama itatokea kampuni moja ikashindwa kutimiza mahitaji yetu, basi tuko tayari kila kitu kitakwenda sawa. Hata sasa kuna unafuu kwani makali ya mgawo yamepungua,” alisema Katyega.
Jana, gazeti hili lilimtafuta Ngeleja kupitia simu zake mbili za kiganjani ili kufahamu msimamo wake kuhusu kuelekea kushindwa kwa mpango wa dharura bila mafanikio.

Hata hivyo, waziri huyo aliwahi kukaririwa akisema hayupo tayari kujiuzulu kwa maelezo kwamba yeye si chanzo cha matatizo ya umeme nchini.
Alisema hayo Julai 19, mwaka huu mjini Dodoma, siku moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuondoa bungeni bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ili iandaliwe upya baada ya kuwa imekataliwa na wabunge.

Kukataliwa huko ndiko kulikozaa mpango wa dharura ambao sasa unaonekana kutotekelezeka hivyo kumweka waziri huyo kwenye wakati mgumu zaidi Bunge litakapokutana tena mwezi ujao.

Ngeleja katika maelezo yake, alisema tatizo la nishati ya umeme ni la Serikali nzima na si yeye peke yake anayepaswa kulaumiwa.


mwananchi.co.tz

0 comments