CHUO Kikuu cha Dar es Salaam, Sehemu ya Mlimani (UDSM), kimewafukuza chuo jumla ya wanafunzi 43 waliokuwa wamesimamishwa masomo wakisubiri kumalizika kwa kesi zilizoko mahakamani pamoja na kuwa viranja wa vurugu zilizotokea chuoni hapo mwanzoni mwa wiki hii.
Aidha, chuo hicho kimewasimamisha wanafunzi tisa kutokana na makosa hayo hayo ambapo wanasubiri uamuzi wa Baraza la Chuo na iwapo watakuwa na hatia, adhabu stahiki itafuatwa.
Kadhalika kimesema kitafanya mawasiliano na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ili wanafunzi waliofukuzwa, wasipate tena mkopo wa Serikali wala kuruhusiwa kudahiliwa tena katika chuo chochote cha umma.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alitoa uamuzi huo jana Dar es Salaam ambo ni wa Baraza la Chuo Kikuu kuhusu vurugu za wanafunzi ambazo zilisababisha uvunjifu wa amani na ukosefu wa utulivu chuoni hapo.
Baada ya kumaliza kusoma uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari, ulibandikwa kwenye kuta za matangazo chuoni hapo na kila mwanafunzi alifika na kusoma.
Kuhusu wanafunzi waliofukuzwa, Profesa Mukandala alisema wako wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu, lakini wengi wa waliofukuzwa ni wa mwaka wa pili na wa tatu na ambao wanasoma masomo ya sanaa.
Profesa Mukandala alifafanua kuwa kati ya wanafunzi 51 waliokuwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Novemba mwaka huu wakikabiliwa na makosa ya kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya Jeshi la Polisi, 43 kati yao ndio waliofukuzwa, watatu sio wanafunzi wa chuo hicho, tisa hawajasikilizwa na Baraza la Chuo hicho na kutolewa mapendekezo.
Aidha, alisema matukio yaliyojiri Jumatatu na Jumanne wiki hii ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoanza mwanzoni mwa Novemba mwaka huu ambapo kila mara vitendo hivyo vilianzishwa na kikundi kidogo cha wanafunzi na hatimaye kupata wafuasi katika kuvuruga shughuli za chuo.
Habari leo
0 comments