Friday, December 16, 2011

MUHASO wasimamisha 66

SIKU moja baada ya Chuo Kikuu cha Dares Salaam kuwafukuza wanafunzi 43, Uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), umewasimamisha masomo wanafunzi 66 kwa tuhuma za kuwa vinara wa vurugu chuoni hapo.

Mbali na hatua hiyo, uongozi wa chuo hicho umeeleza kuwa mipango ya vitisho na uvunjifu wa amani chuoni hapo, bado ipo na inaleta hofu kwa walimu na wanafunzi wengine wanaoendelea na masomo.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kisali Pallangyo, alisema jana kuwa wanafunzi waliosimamishwa ni wale waliohusika katika vurugu zilizotokea chuoni hapo Desemba 8, mwaka huu wakati wa sherehe ya utafiti na Desemba 10 wakati wa mahafali na Jumatatu wiki hii.

Profesa Pallangyo alisema wanafunzi hao wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana hadi hapo uchunguzi utakapokamilika na kwamba matokeo ya uchunguzi huo ndio yatakayoamua kama wanafunzi hao waendelee na masomo au la, alisema.

“Tunao ushahidi kwamba wamefanya makosa, lakini na wao watapewa nafasi ya kuja kujitetea na inawezekana idadi hiyo ikaongezeka na tutatumia taratibu za ndani za kinidhamu,” alifafanua Profesa Pallangyo.

Alisema kati ya wanafunzi hao ambao ni wa mwaka wa tatu na wa tano kuna msichana mmoja tu mmoja aliyekumbwa na adhabu hiyo.

Aliongeza kwamba, uongozi wa chuo hicho una ushahidi wa mkanda wa video na taarifa zingine kutoka vyombo vya usalama.

Alieleza kuwa chanzo cha vurugu hizo ni madai ya wanafunzi hao kutaka kurejeshewa serikali yao wanafunzi (Muhasso) iliyovunjwa na Baraza la chuo hicho.

Profesa Pallangyo alisema shughuli za serikali hiyo zilisitishwa tangu Juni mwaka huu na baraza la chuo hicho kutokana na kukaidi maagizo ya Serikali yaliyotaka vyuo vikuu vyote kubadili katiba zao.

Kwa mujibu wa Profesa Pallangyo, mwaka 2009 serikali ilitoa waraka kwa serikali za wanafunzi katika vyuo vikuu vyote kwamba wabadilishe katiba zao, lakini serikali nyingi za wanafunzi ikiwemo Muhasso, hawakukubaliana na uamuzi huo.

“Tuliongea nao kwenye baraza la chuo na kuwashawishi wabadili katiba yao ili iendane na waraka wa serikali, lakini walikataa na Februari mwaka huu Waziri wa Elimu alikuja hapa na kuzungumza nao lakini walikataa,” alisema.

Makamu Mkuu huyo alisema vyuo vingine kama Dodoma, Mzumbe na Mkwawa walikubali kubadilisha katiba zao lakini Muhasso waliendelea na msimamo wao wa kukataa.

Alisema baada ya baraza la chuo kusitisha shughuli za Muhasso, Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi, Gervas Shayo alikwenda mahakamani kufungua kesi akiwashtaki Makamu Mkuu wa chuo hicho, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambayo hukumu yake haijatolewa.

Alisema uongozi wa chuo uliwataka wanafunzi hao waiondoe kesi mahakamani ili wakae na kujadiliana namna ya kurejesha Muhasso, lakini bado walikataa na kwamba, waliharibu sherehe za utafiti pamoja na mahafali.

Alisema pia vurugu hizo zinaweza kuwa na athari kubwa hasa kwa wafadhili wao wakubwa ambao ni serikali ya Sweden, ambao walikuwepo Desemba 8, wakati wa sherehe ya utafiti chuoni hapo.

Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eligius Lyamuya alisema mipango ya kutishia amani bado ipo chuoni hapo na kwamba, inaleta hofu kwa walimu na kwa wanafunzi ambao wako tayari kuendelea na masomo.


mwananchi

0 comments