Theopista Nsanzugwanko
SERIKALI imesema itahakikisha king’amuzi kimoja kinaonesha vituo vyote vilivyo nchini pamoja na vituo hivyo kuendelea kuonekana hata baada ya malipo ya mwezi kuisha.
Aidha, nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu saa sita kamili usiku, vituo vyote vya utangazaji vinavyotumia teknolojia ya analojia vitalazimika kuzima mitambo yake na kuanza kurusha matangazo hayo katika mfumo wa digitali pekee.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa kuhusu usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia na kuhamia teknolojia ya digitali.
Profesa Mbarawa alisema baada ya mabadiliko hayo kutokana na uhitaji mkubwa wa ving’amuzi watahakikisha vinashuka bei ikiwamo pamoja na kuongezeka kwa kampuni ya simu za mkononi, jambo litakalofanya kuongezeka kwa kodi na bei ya matumizi ya simu kushuka.
Alisema vituo vya ndani ya nchi kuonekana hata malipo ya mwezi yakiisha ni haki kutokana na kuwa havina malipo na kutoonekana kwa sasa ni kutokana na changamoto ya kutoka teknolojia moja kwenda nyingine.
Alisema kuhamia katika mfumo wa digitali kutasaidia kupunguza matumizi ya masafa hivyo kuwa na zaidi ya masafa 670 hadi 862, hivyo kuwekeza katika simu za mkononi, jambo litakaloongeza kodi na gharama za simu kupungua.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Florens Turuka alisema suala la king’amuzi kimoja kuonesha vituo vyote vya ndani ni la kitaalamu ambalo limejadiliwa katika mikutano ya nchi za Afrika Mashariki na ule wa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC).
Alisema wataalamu wanalishughulikia suala hilo ambalo litakamilika kabla teknolojia ya analojia haijafungwa rasmi nchini jambo litakalowasaidia watangazaji kupata wateja kutokana na kupata watazamaji wengi.
Aidha, Serikali kupitia Wizara yake pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), watahakikisha kuwa mabadiliko hayo yanafikiwa bila kuathiri teknolojia na mifumo mbalimbali ya mawasiliano iliyopo nchini.
0 comments