Sunday, May 27, 2012

Zanzibar Ina Historia Yake, Tanganyika Je?

Na Nova Kambota

Miaka minne imepita tangu mwandishi maarufu wa makala nchini Bwana Hussein Siyovela alipoandika makala akihoji “Wazanzibar wanategemea nini nje ya Muungano?” akiwahoji Wazanzibar kama wanafahamu athari za kuwa nje ya Muungano ama la?.

Naye mwandishi mwingine Bw Prudence Karugendo ameandika akimjibu Siyovela katika makala iliyokuwa na kichwa cha habari “Wazanzibari wanategemea Muungano Imara”.

Hawa ni waandishi wawili walioonyesha mitazamo tofauti, huku Bw Siyovela akionyesha dalili za kuwatisha Wazanzibar, mwenzake Karugendo ameonyesha jinsi Wazanzibar wanavyoelewa kile wanachokipigania. Labda ambacho Karugendo amesita kukiweka wazi ni jinsi Watanganyika walivyo kimya kwenye hoja ya muungano kiasi cha kutoa picha ama hawajui waseme nini? au hawaujui muungano wenyewe?.

Nitajadili hili leo….. Tukiachana na haya “mazingaombwe” ya watawala ya kutaka tuandike katiba mpya pasipo kuujadili muungano na “porojo” nyinginezo, acha niwapongeze wazanzibar kwa msimamo wao kuhusu muungano, nayasema haya kutokana na uzalendo mkubwa wa watu wa visiwa hivi wa kusema ukweli kutoka moyoni kwao kuwa tujadili muungano kwanza halafu mengine baadae, hali ni tofauti kwa watanganyika ambao wako kimya utadhani muungano hauwahusu, hii ni ajabu sana!

Nitaendelea kushangaa kutokana na ukimya wa Watanganyika huku wenzao Wazanzibar wanatamba kila jukwaa wakiichambua kwa uzuri kabisa kile kinachoitwa historia ya “Zanzibar Empire”, naendelea kushangazwa na ukimya huu wa Watanganyika ilihali wenzao Wazanzibar wameanza hata kupendekeza aina ya muungano wanaoutaka, huku baadhi wakitaka muungano wa kimkataba na wengine wakitaka serikali tatu.

Najiuliza nani kawaziba midomo watanganyika? Hivi huu ni ukimya au kuna la zaidi hapa? Iwapo mkimbizi mwenyewe hasiti kujitambulisha, iweje leo watu walioadhimisha miaka hamsini ya uhuru hawataki kujadili historia yao!….no there must be some motivations behind, lazima kuna namna tu, si bure!.

Hivi leo ni Mtanganyika gani mwenye ujasiri wa kutueleza historia ya Tanganyika? Nasema historia huru ya Tanganyika, sitaki kusikia upuuzi wa kina John Heaning Speak na kugundua mlima Kilimanjaro!, kwa maana nacho kiona sasa ni historia ya wazungu ndani ya Tanganyika kubatizwa na kuitwa historia ya Tanganyika, huu mzaha!

Sijui utadumu mpaka lini? Labda niseme hivi, ingekuwa ni tofauti baina ya wanandoa tungewaachia wenyewe, lakini hili linahusu maslahi mapana ya taifa na watu wake, na kwa vile ni mmoja wa wananchi wa taifa hili lazima nipaze sauti katika hili.

Haiwezekani tukajifanya “wehu” kwa kukataa ukweli kuwa kwa jinsi hali ilivyo sasa ni kama vile Zanzibar wana historia yao, wanajivunia, wanaiongea waziwazi, na wanajua wanachokitaka tofauti na watanganyika ambao ukimya wao unazidi kuwaduwaza walimwengu.

Kwa tuliobahatika kufika Zanzibar tunafahamu jinsi Wazanzibar wanavyodumisha utamaduni wao, nathubutu kusema isingelikuwa wahamiaji wahuni visiwani humo leo hii msamiati “wizi” na “uchangudoa” ungefutwa kwenye kamusi yao, sasa nani hafahamu Shiva Arusha au Buguruni na Manzese nini kinatokea? nani hajui kuwa Wazanzibar wapo tayari kujipambanua kokote kwa misingi ya tunu zao hizi, au tuseme Watanganyika wamepigwa na mawimbi ya ubepari kiasi cha kupoteza tamaduni zao?

Kuna nini hapa?
Halafu anaibuka mtu asiyetaka kuuona ukweli huu na kuwapakazia dhambi ya ubaguzi Wazanzibar, huu ni upuuzi! Hivi nani kakataza Watanganyika kueleza historia yao? Au lini mtu kujitambulisha ikawa ubaguzi? Eti nimesikia kilio cha samaki kuwa “ubaguzi ni dhambi kama baba wa taifa alivyowahi kuasa” ni kweli ubaguzi dhambi! Lakini nani mbaguzi? , imefika wakati watanganyika waache kukimbia kivuli chao, waache kumung’unya maneno badala yake wajivunie historia yao, kuliko kutaka kuwatisha wazalendo wa Zanzibar.

Kwa nukta hii sasa, wakati nawapongeza Wazanzibar kwa uzalendo wao na historia yao tamu isiyochosha masikio, nawataka Watanganyika waache vitisho vya kusadikika kuhusu ubaguzi, badala yake waiambie dunia pasipo uwoga kuwa na wao wana historia yao tena tamu kama asali, kinyume cha hili, nitaendelea kuamini kuwa Wazanzibar wanajielewa huku Watanganyika wanajikana wenyewe!


Tafakari! A luta continua!
Nova Kambota ni mwandishi na mchambuzi wa maswala ya kisiasa, anapatikana kwa anwani ya barua pepe novakambota@gmail.com, au waweza kutembelea tovuti yake www.novakambota.com

No comments:

Post a Comment