KATIBU mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamis Suleiman Dadi (kulia) akimkabidhi fomu za kuwania nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hiyo |
MDAU wa michezo nchini
Abdallah Majura Bulembo amejitosa kuwania uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa
wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Bulembo ambaye aliwahi kuwa
mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara (MRFA) na mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alichukua fomu hizo na
kuzirejesha jana hiyohiyo.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hizo, Bulembo alisema kwamba
amelazimika kuwania nafasi hiyo ili kuifanyia makubwa jumuiya hiyo kwani ni mwanachama
halali wa CCM na mwenye sifa hivyo anawajibu wa kuwania nafasi yoyote inayomfaa
kwa lengo la kuendeleza mikakati iliyopo ndani ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Bulembo ambaye
katika uchaguzi uliopita aligombea nafasi hiyo na kushika nafasi ya pili nyuma
ya Balozi Athuman Juma Mhina ambaye sasa ni marehemu, alisema ataweka wazi
mikakati yake pindi atakapopitishwa na halmashauri kuu ya CCM.
Bulembo anakuwa mgombea wa
saba kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo ambapo awali wanachama waliojitosa ni
pamoja na John Edward Machemba, Said Ramadhan Bwanamdogo, Salim Hamis Chikago,
Jasson Samson Rweikiza, Alfred Joseph Mwambeleko na Alphonce John Siwale.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya
hiyo Hamis Suleiman Dadi,alisema zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu wa
nafasi mbalimbali katika jumuiya hiyo lililoanza Agosti 22 litafikia tamati Agosti 29 mwaka
huu.
Alisema mbali na nafasi ya
uenyekiti, tayari baadhi wa wanachama wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongoizi katika
jumuiya hiyo kwa upande wa Bara na Visiwani.
Alizitaja nafasi nyingine ni
pamoja na Baraza Kuu la Wazazi Bara na Zanzibar, Wajumbe wa Kamati Kuu Wazazi kwa
upande wa Bana na Visiwani, Jumuiya ya Wazazi kwenda Umoja wa Wanawake (UWT)
na Jumuiya ya Wazazi kwenda Umoja wa
Vijana (CCM).
mwisho
0 comments