Friday, August 17, 2012

Falsafa muhimu ya Zakatul Fitri kwa Mwislamu

Hassan Rashidi

SALAAM Aleikum mpenzi msomaji, ikiwa ni mara nyingine tunakutana katika Ijumaa hii ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani katika mwaka huu 1433 Hijiria.
Tukiwa katika kuelekea kumaliza mwezi wetu na kuwa na maandalizi ya kuadhimisha Sikuu ya Idd el - Fitri, ambapo tunaangazia umuhimu wa utoaji wa Zakaatul-Fitri kwa Mwislamu.

Zakaatul - Fitri ni nini?

Zakaatul-fitri ni kile chakula anachokitoa mtu mwishoni mwa mwezi wa Ramadhani na kuwapa wanaostahili kupewa zaka kabla ya swala ya Idd el-Fitri.

Nini hukumu yake?

Zakaatul-Fitri ni faradhi mbele ya kundi kubwa la wanazuoni. Ufaradhi huu unatokana na hadithi iliyopokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi - yeye amesema:

“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-Amefaradhisha Zakaatul-Fitri ya Ramadhani. Pishi la tende au pishi ya shayiri, kwa mtumwa na muungwana, mwanamume na mwanamke, mtoto na mkubwa katika Waislamu. Na ameamrisha itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali (yaani swala ya Eid).” Bukhaariy & Muslim.

Mtume Muhammad (S.A.W), ameifaradhisha Zakaatul-Fitri na kuamrisha itolewe katika mwaka ule ule uliofaradhishwa swaumu ya Ramadhani. Yaani katika mwezi wa Shaaban, mwaka wa pili wa Hijrah.

Nini falsafa yake?

Zakaatul-Fitri imefaradhishwa kwa hekima nyingi, miongoni mwake ni kuwasaidia wenye shida katika siku ya sikukuu ili furaha ienee kwa watu wote.

Lengo la kufanya hivyo ni kuunga upungufu na kuziba makosa yanayoweza kuwa yamemtokea mtu katika swaumu yake.
Haya tunayafahamu kupitia hadithi ya Ibn Abbas-Allah awawiye radhi kwamba yeye amesema:

“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie, alifaradhisha Zakaatul-Fitri ili kumtwaharisha mfungaji kutokana na maneno na matendo machafu. Na ili iwe chakula kwa masikini, atakayeitoa kabla ya swala basi hiyo ndiyo zaka yenye kukubaliwa. Na atakayeitoa baada ya swala, basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyinginezo.” Abuu Daawoud.

Inamuwajibikia nani?

Zakaatul-Fitri ni wajibu kwa kila Mwislamu, mwenye uwezo wa kutoa hata kama hamiliki kiwango cha zaka ya fardhi. Mwenye kumiliki chakula chake na familia yake cha siku ya Idd, kinachozidi hapo ni wajibu akitoe kama Zakaatul-Fitri.

Atajitolea yeye mwenyewe na watu wote ambao chakula chao cha kila siku kinamuwajibikia yeye. Hawa ni pamoja na wanawe ambao bado wanamtegemea yeye, wazazi wake, mkewe na wale wote walio chini ya ulezi wake kwa njia ya wajibu na wala si kwa njia ya ihsaani/ hiyari.

Nini kitolewacho?

Zimepokewa hadithi nyingi sahihi zinazoweka wazi alichowaamrisha mtume zimshukie-maswahaba wake kukitoa kwa ajili ya Zakaatul-Fitri.

Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokewa kutoka kwa Abuu Saaid Al-khudriy-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tulikuwa wakati alipokuwa miongoni mwetu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-tukimtolea Zakaatul-Fitri kila mkubwa na mdogo. 

Kibaba cha chakula, au kibaba cha shayiri, au kibaba cha zabibu au kibaba cha maziwa ya unga.” Bukhaariy.

Abdillah Ibn Tha’alabah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie alihutubia siku moja au mbili kabla ya Eid.

“Toeni kibaba cha ngano, au kibaba cha tende au cha shayiri. (Mtoleeni) kila muungwana au mtumwa, mkubwa au mtoto.” Abuu Daawoud.

Mafaqihi wamesema mazingatio katika kutoa ni kuangalia chakula rasmi cha mahala husika, chakula kitumiwacho katika dhifa na shughuli zao mbalimbali.

Na kibaba kwa kipimo cha kilogramu ni sawa na ¾ ya kilogramu moja. Hiki ndicho kipimo kinachopaswa kutolewa kwa kila kichwa kimoja.

Itolewe nini?

Wakati bora kabisa wa kutoa Zakaatul-Fitri ni ule usiku wa kuamkia siku ya Idd. Na ni wajibu itolewe kabla ya kuswaliwa swala ya Idd. Na wajibu wa kutoa haupomoki/hauondoki kwa sababu ya kuchelewa kutoa.

Bali itakuwa ni deni iliyo katika dhima ya aliyewajibikiwa kutoa. Na itamlazimu kulipa deni hilo hata mwishoni mwa umri wake, kwa sababu aliwajibikiwa na akafanya uzembe kutoa.

Na haiswihi kuchelewa kutoa bila ya dharura na ni haramu kisheria. Kwa sababu ucheleweshaji huu unasababisha kupotea kwa lengo la utoaji wake ambalo ni kuondosha uhitaji wa maskini katika siku ile ya furaha.

Apewe nani?

Wanaopaswa kupewa Zakaatul-Fitri ni wale wale wenye sifa ya kupewa Zaka ya faradhi ambao wametajwa katika kauli yake Allah.

“Sadaka hupewa (watu hawa); maskini na wanaozitumikia nyoyo zao juu ya Uislamu na katika kuwapa uungwana watumwa na katika kuwasaidia wenye deni na katika kutengeneza mambo aliyoyaamrisha Allah hasa kwa kupewa wasafiri walioharibikiwa, ni faradhi inayotoka kwa Allah na Allah ni mjuzi na mwenye hekima.”

0 comments