Friday, August 3, 2012

HOJA NA MAONI YA WAISLAMU JUU YA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO YA TANZANIA

Katika zoezi la kukusanya na kuwasilisha maoni ya Waislamu juu ya Katiba Mpya vipo vyombo viwili kwa ajili ya Waislamu, vyote vikiwa na azma moja, kulinda na kutetea maslahi ya Uislamu na Waislamu nchini. Vyombo hivi ni:

1. Jukwaa la Waislamu la Kuratibu Mabadiliko ya Katiba Tanzania (JUWAKATA)
2. Mtandao wa Misikiti Tanzania

JUWAKATA imekwishatoa maelekezo muhimu kwa Waislamu katika kijitabu chenye anuani “MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA”. Jukwaa limefanya kazi kubwa ya kupita katika mikoa mingi nchini kutupa maelekezo muhimu na mambo ambayo Waislamu hatuna budi kuyapigania yawepo katika Katiba Mpya. Mtandao wa Waislamu wa Mawasiliano na Kupashana Habari umepata nakala ya kijitabu hiki chenye kutoa maelekezo kwa Waislamu.

Mtandao wa Misikiti Tanzania umetoa MUHTASARI WA HOJA NA MAONI JUU YA KATIBA MPYA kama yalivyokusanywa na kuratibiwa kutoka katika semina shirikishi za mtandao wa misikiti nchini. Semina hizi zimefanyika katika mikoa 17 Tanzania Bara na mkoa mmoja Zanzibar. Mtandao wa Waislamu wa Mawasiliano na Kupashana Habari umepata nakala ya kabrasha lenye hoja na maoni haya.

Waislamu hatuna budi kuwasilisha maoni yetu kama KUNDI MASILAHI na sio kama Watanzania, au watu wa wilaya, mkoa fulani au wa kundi la aina yoyote katika jamii ambalo halijinasibishi moja kwa moja na Uislamu. Katika kufikia lengo hili Mtandao umeambatanisha katika waraka huu MUHTASARI WA HOJA NA MAONI YA WAISLAMU JUU YA KATIBA MPYA. 

Nia na madhumuni ya kiambatanisho hiki ni kutoa fursa kwa Waislamu katika kila kona ya nchi yetu ya kutoa maoni haya kwenye Tume ya Taifa ya Kukusanya Maoni moja kwa moja kupitia E-Mail Address ya Tume (Anuani ya Tume ya Barua Pepe).

 Unaweza kuchagua idadi yoyote ya hoja na maoni (kwa jozi ya pamoja) na kuyatuma kwenye Tume kwa anuani ifuatayo: Email : maoni@katiba.go.tz

Ili maoni yako yapate tafsiri ya kutumwa na Muislamu kwa ajili ya Uislamu huna budi kujitambulisha kwa:

· Jina lako
· Mawasiliano ya Simu (kama una simu)
· Msikiti Wako Unakoswalia (Muhimu Sana)
· Wilaya na Mkoa (Ulipo Msikitin wako)

0 comments