Monday, August 13, 2012

UMUHIMU WA SWALA

Bismillahi-Rrah
mani-Rrahim. Alhamdulillahi Rabbil Aalamiyn, waswalatu wassalam ‘alaa RasuliLlaahi. Amma ba’ad.

Assalamu ‘Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh.



}}وَأَقِمِ الصَّلاَةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّـيِّئَاتِ ذَلِكَ ذِكْرَى لِلذَّاكِرِينَ{
{

{{Na shika Swalah katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka}} (11:114)

}}وَاسْتَعِينُو
اْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاَةِ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلاَّ عَلَى الْخَاشِعِينَ{{

{{Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu}} (2:45)

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ameturuzuku zawadi kubwa ambayo thamani yake haina mfano. Lakini kwa ajili ya uzoefu wetu juu yake, mara nyingi hatuipi cheo na heshima inayostahiki zawadi hiyo. Zawadi hiyo yenye thamani kubwa ni Swalah. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituletea zawadi hii kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) alipopelekwa kwenye mbingu saba katika safari yake ya Mi’raaj. Kama tujuavyo, kwanza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa Swalah khamsini ambazo zilipunguzwa mpaka tano, zile tunazoziswali sasa; na kwa Ukarimu Wake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) tunapata fadhila ya zile Swalah khamsini vile vile, ilihali tunaswali tano. Subhana Allaah!

Kwa hivyo Swalah yetu, ambayo wengi wetu tunaichukulia kwa wepesi na kuipuuza, ina utukufu wa kukutana kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Inasemekana kuwa yale maneno tunayoyasema katika tashahhud ni kumbukumbu ya mawasiliano yaliyotokea baina ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Mola wake wakati huo wa Mi’raaj. Wa Allaahu A’alam. Kwa hivyo, kila tunapokaa kwenye tashahhud, inatupasa tuwe ni wenye kuzingatia utukufu wa kikao hicho.

Swalah ni mojawapo ya njia kubwa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametutolea iwe ni hakikisho kuwa tunabaki kwenye njia ya Uislamu ambayo inaongoza kwenye Rehma Yake na Msamaha Wake, na kila zuri duniani na Aakhira. Kwa hakika, Swalah inatuunganisha na Mola wetu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelinganisha Swalah na mto ambao mtu akioga ndani yake mara tano kwa siku, Hakika mtu huyo hatokuwa mchafu. Hivyo basi, Swalah zetu tano zinazuia kufungika kwa uhusiano baina yetu na Allaah. Kwa hivyo kuswali kwetu, daima kunafuta madhambi madogo yaliyotendeka baina ya kila Swalah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametufaradhishi
a Swalah ili daraja zetu zipande, thawabu zetu zizidishwe, na madhambi yetu yadondoke kutoka kwetu, na kwa ajili yake Atutie Peponi na Atuokoe na Moto.

Walakini, Swalah ni kama upanga wenye makali pande zote mbili. Tukiihifadhi, itatupa mwangaza kwenye nyoyo zetu, makaburi yetu, na siku ya Kiama. Itatushuhudia wakati ambao tunahitaji shahidi ili tuokoke na adhabu ya Moto, kama tujuavyo kutoka kwa Yahya ibn Sa'id kwenye Muwatta: “kitendo cha kwanza kutizamwa siku ya Kiama ni Swalah, ikikubaliwa, basi vitendo vyengine vitaangaliwa, lau sio hivyo, basi vitendo vyote pia havitoangaliwa.
” Lakini tukiipuza na kuitoa thamani, basi nayo itatoa ushahidi dhidi yetu, wakati ambao tunahitajia shahidi zaidi. Lazima tujihadhari tusiwe miongoni mwa watu wale ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) anawazungumzia katika Surat Maryam:

}}فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا{{

{{Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha Sala, na wakafuata matamanio. Basi watakuja kuta malipo ya ubaya}} (19:59)

Na tuzingatie maneno ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) : Jabir amesema, “nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema,

((Kitu ambacho kinasimama baina ya binaadamu na kutokuamini na shirki, ni kuacha Swalah)) [Muslim]

Cheo cha Swalah katika dini ni kama mfano wa mlingoti wa nyumba, ukiwepo, nyumba itakuwa madhubuti na vifaa vyake vyote vitalingana mahali pake. Lakini isipokuweko, basi jengo lote litabomoka na kuwa halina maana.

Kulingana na hayo, ni muhimu kukumbuka kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hatuamrishi kuswali tu, bali Anatuamrisha tuimarishe Swalah, ambapo Mufassirun wote wamekubaliana kuwa kuimarisha Swalah, ina uzito zaidi kuliko kuswali tu rakaa tulizoambiwa. Kuimarisha Swalah ina maanisha shuruti zote za twahara, mahali pa kuswali, nguo, kibla, na mengineyo, yote ni lazima yatimizwe.

'Abdullaah bin Mas'uud amesema, "Yeyote anayetamani kukutana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kesho, basi atunze Swalah hizi tano wakati muadhini unapoadhini Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Alimuonesha Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Sunnah zote za muongozo, na kuimarisha Swalah ni moja wapo. Ukiswali nyumbani kwako kama wanao kosa kuswali jama’a, umetupilia mbali Sunnah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) . Na ukitupa Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) , huwezi kuongoka. Mumetuona sisi, na hakuna kati yetu ambao walikosa Swalah ya jama’ah isipokuwa wale wanafiki ambao unafiki wao ulikuwa unajulikana, au wale waliokuwa wagonjwa. Watu walikuwa wanakuja kuswali jama’ah huku wameshikiliwa na watu wawili mpaka wakasimamishwa kwenye safu”.

Swalah ni kitu ambacho hakiwezi kumalizwa kuzungumziwa, na vitabu vingi vimeandikwa juu yake, lakini ningependa kumalizia kwa kauli zifuatazo walizosema baadhi ya Maulamaa waliotangulia, kuhusu Swalah:

1)

"Kwa vile Allaah Anajua kuwa munachokeshwa na kitu mara moja,

Amezifanya namna kwa namna ibada zenu juu Yake.

Kwa vile Anajua kuwa muna pupa,

Amewakataza kuzifanya Ibada wakati mwengine.

Amefanya hivyo ili matamanio yenu yawe ni kuimarisha Swalah,

Sio kuswali tu!

Sio wote wenye kuswali wanaimarisha Swalah.

Swalah ni utakaso wa nyoyo,

Na mahali pa mazungumzo ya undani,

Baina ya mja na Mola wake.

Viwanja vya siri vinaenea ndani yake,

Mianga inaangaza na kumulika nuru zake.

Allaah Anajua nyinyi ni dhaifu,

Basi Amezifanya idadi za Swalah kidogo tu!

Anajua kuwa nyinyi ni wahitaji wa Rehma Zake nyingi.

Kwa hivyo amezidisha Neema Zake kwenu ndani yake"



2)

"Yeyote anayetamani kujiokoa nafsi yake, kujifurahisha moyo wake, kusitiriwa makosa yake, kupata Radhi za Mola wake, na moyo wake kupata uhai, lazima ampe heshima Anayostahiki Mola wake na asicheleweshe Swalah wakati unapoingia, na asijiruhusu kufanya hivyo. Wala asiswali peke yake wakati ambao anaweza kuswali jama’ah. Na bado tunaona watu wakichelewesha Swalah na kuswali peke yao ilihali wanaweza kuswali jama’a. Ni ubaya ulioje wanaoufanya hao. Tunawaona wamezama ndani ya mhangaiko, huzuni, taabu, na mateso. Hakika, chanzo cha yanayowapata ni kupuuza kwao kwa dini. Pia tunaona kuwa hawajui tofauti ya kuswali safu ya mbele wala ya nyuma. Sio kwa sababu hawajui, bali ni kwasababu ya kutojali dini. Hawajali kuhusu twahara pia. Lakini ukweli ni kuwa, yeyote mwenye najisi, hana udhu, na ambae hana udhu, hana Swalah, na ambae hana Swalah, hana mazuri yoyote. Wa Allaahu A’alam"



3)

"Kuna nuru kubwa katika Swalah ambayo inaangaza ndani ya nyoyo za wale wanaoimarisha swala na wale wanaomakinika na kunyenyekea kwenye Swalah zao. Kwa hivyo, ukija kuswali, komboa moyo wako kutokana na dunia na vilivyomo ndani yake; jihusishe na kumakinika na hudhurio la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ambaye Swalah hiyo ni kwa ajili Yake. Lazima ujue kwamba msingi wa Swalah ni unyenyekevu na kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kusimama, kurukuu, na kusujudu mbele Yake, na Kumtukuza kwa takbir, tasbih, na dhikri.

Kwa hivyo tunza Swalah yako kwa sababu ni ibada kubwa kabisa miongoni mwa ibada. Usimuache shetani acheze na moyo wako na kukupurukusha katika Swalah ili usipate utamu wa nuru ya Swalah. Na muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani Yeye ndiye Mbora wa Wasaidizi".



Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaaliye tuwe miongoni mwa waja wake ambao wanathamini ile zawadi Aliyotupa ndani ya Swalah. Tunamuomba Atuongezee unyenyekevu na utulivu ndani ya Swalah ili tuwe ni wenye kufaidika nayo. Tunaumuomba Allaah Atulete pamoja ndani yake (Swalah) na atuzidishie idadi ya safu na atupe nguvu ndani yake (Swalah) ili tutoke ndani yake ilihali tumenufaika. Aamiyn.

0 comments