Monday, November 21, 2011

Wabunge CCM walalama mkutano wao na Kikwete

BAADHI ya wabunge wa CCM wamelalamikia mkutano ulioitishwa baina yao na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kwamba haukuwa na tija tofauti na matarajio makubwa waliyokuwa nayo.

Rais Kikwete, juzi usiku alikutana na wabunge wa chama chake katika Ukumbi wa St. Gasper nje kidogo ya Mji wa Dodoma lakini habari zilizopatikana jana zilisema mkutano huo uligeuka kuwa wa “chakula cha jioni.”

“Mkutano wenyewe haukuwa na tija, kwanza tulisubiri sana hadi watu wakaanza kukata tamaa, lakini hata Rais alipofika hakukuwa na mkutano kama tulivyoambiwa na badala yake tuliambiwa ni dinner tu (chakula cha usiku) halafu mazungumzo ni siku nyingine,” alisema mmoja wa wabunge aliyehudhuria hafla hiyo.

Mbunge mwingine alisema: “Wengine tulikuwa tumejipanga kumuomba Rais achukue hatua kuhusu mambo yanavyokwenda ndivyo sivyo, serikalini na kwenye chama, lakini ndiyo hivyo, haikuwezekana, maana tuliishia kula na baadaye kutawanyika.”

Usiku huo, Rais Kikwete alitoa hotuba fupi yenye sura ya salaam kwa wabunge hao huku akiwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya bungeni na kwa ujasiri wao wa kutokuwa wanyonge kwenye mijadala bungeni.

Kikwete alinukuliwa na vyanzo vyetu akiwapongeza wabunge wa CCM kwa jinsi walivyoutetea Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2011 pamoja taarifa za Kamati mbili za Bunge zilizowasilishwa kuhusu sekta ya gesi na ile ya Kamati Teule.

Mbunge mwingine aliyezungumza na gazeti hili alisema: “Sisi ndiyo tulimwomba Rais aje kuzungumza nasi, lakini hatujui ni nini kilichotokea, tumeahidiwa kwamba huenda akaja kusema na sisi tutakapokutana mwezi Februari mwakani.”

Kwa mujibu wa mbunge huyo, walikuwa wamejiandaa kuzungumzia matatizo ya nchi hasa kuyumba kwa uchumi, hali ngumu ya maisha na udhaifu katika utendaji wa Serikali ambao umekuwa ukiwaweka katika wakati mgumu kuwakabili wapinzani bungeni.

“Mambo hayaendi kabisa, watendaji serikalini ni kama hawaoni, sasa tulidhani kwamba fursa hii ilikuwa ni ya kumshauri Rais aweze kuchukua hatua zaidi, vinginevyo tutakwama, hatuna matumaini kadri siku zinavyokwenda,” alisema mbunge huyo.

Jitihada za kumpata Mwenyekiti wa Kamati ya wabunge wa CCM, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na katibu wa kamati hiyo, Jenister Mhagama (Mbunge wa Peramiho), kuzungumzia mkutano huo hazikufanikiwa.

Taarifa rasmi kutoka Ikulu ilisema Rais alizungumza na wabunge wa CCM kisha kupata nao chakula cha usiku katika ukumbi wa St. Gasper.

Taarifa hiyo ilisema Kikwete aliwapa changamoto wabunge hao kwenda kwa wapiga kura wao kuwaelimisha kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Taarifa hiyo imemnukuu Mwenyekiti huyo wa CCM akiwasisitizia wabunge hao umuhimu wa kutoa elimu kuhusu suala hilo, kutokana na kuwapo kwa upotoshaji unaofanywa kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge.

Soma zaidi

0 comments