KAMATI ya Kutetea Haki za Waislamu nchini, imeihadharisha Serikali kutojihusisha na mambo ya kidini hasa yanayohusu kundi la Al-shaabab kwa shinikizo la mataifa makubwa.
Katibu wa kamati hiyo, Shekhe Ponda Issa Ponda, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kamati hiyo imemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, kupinga kauli yake aliyowataka Watanzania kuwa makini na wahamiaji haramu ili kudhibiti kundi hilo lisiingie nchini.
Shekhe Ponda alisema ni vyema Serikali ikawa makini na sera za mataifa makubwa ambayo yameingia katika migogoro na baadhi ya nchi za Afrika kwa maslahi binafsi.
“Serikali iache kujiingiza katika migogoro na kundi hili, jambo la msingi ni kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu si vinginevyo,” alisema Shekhe Ponda na kuongeza kuwa, si kweli kwamba kundi hilo ni la kigaidi kama alivyosema Bw. Nahodha bali kinachofanywa na kundi hilo ni kulinda mipaka ya nchi yao.
Alisema Bw. Nahodha hapaswi kuwaweka Watanzania katika hofu ya kuvamiwa na kushindwa kusafiri kwa shughuli mbalimbali ambazo ndizo huwapatia kipato na kukuza uchumi wao kutokana na taarifa za upotoshwaji dhidi ya kundi hilo.
“Waziri anapozungumzia kundi hili ni sawa na kudhalilisha Uislamu, mbona hivi karibuni wameingia Wakongo wakiwa na silaha nzito lakini Serikali haikufanya kitu, kwanini Al- Shaabab,” alihoji Shekhe Ponda.
Bw. Ponda alisema kauli iliyotoa Bw. Nahodha, imelenga kuwagawa Watanzania ili waichukie nchi ya Somalia kitu ambacho si sahihi.
Hivi karibuni, Bw. Nahodha alisema kutokana na nchi jirani ya Kenya kukumbwa na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na kundi hilo, umefika wakati wa Watanzania kuwa makini na watu ambao wanaingia nchini kinyemela bila kufuata utaratibu
Majira
0 comments