Thursday, December 29, 2011

SIMULIZI: MOLA WAKO MLEZI ATAKUPA MPAKA URIDHIKE

Baada ya kumaliza masomo yangu ya chuo kikuu nilipata kazi nzuri sana. Wachumba wakaanza kuja kunichumbia. Lakini hakuna niliye ridhika nae ili awe mshirika wangu wa maisha.

Kisha baada ya hapo nikashughulishwa sana na kazi mpaka nikasahau kabisa masuala ya ndoa. Mpaka nikafikia umri wa miaka 34. Nikaanza kupata shida kutokana na kuchelewa kwangu kuolewa.

Siku moja akajitokeza kijana mmoja kunichumbia, na alikuwa akinizidi kiumri kwa miaka miwili. Hali yake ya kimaisha ilikuwa ni mbaya lakini niliridhika nae juu ya hali hiyo.

Tukaanza maandalizi ya ndoa, akaniomba fotocopy ya kitambulisho changu, nikampatia. Baada ya siku mbili mama yake akanipigia simu, akanitaka nikutane naye haraka kadri iwezekanavyo.

Nikaelekea nyumbani kwake, ghafra nikashangaa ananitolea ile fotocopy ya kitambulisho changu. Akaniuliza: Hivi tarehe ya kuzaliwa katika kitambulisho chako ni sahihi?! Nikamjibu: Ni sahihi.

Akasema kwa hiyo wewe wakaribia miaka arobaini?! Nikamwambia mie nina umri wa miaka 34.

Akasema: Hakuna tofauti wewe ushavuka miaka therathini, na matarajio ya kuzaa ni madogo sana, na mie ninataka kuwaona wajukuu zangu.

Mambo hayakutulia mpaka uchumba wetu ukavunjika. Ukapita muda wa miezi sita ambayo ilikuwa ni migumu sana kwangu.

Nikaamua nielekee Umra ili niweze punguza fikra na mawazo katika nyumba tukufu ya Allah.

Nikaelekea katika nyumba tukuf ya Allah (Masjidi al haraam). Nikawa nikiswali hali ya kuwa ni mwenye kulia nikimuomba Allah na kumshtakia anifanyie wepesi na ajaalie kheri juu ya suala langu la ndoa.

Pindi nilipo maliza kuswali, nikamuona mwanamke mmoja akisoma Qur ani kwa sauti nzuri. Alikuwa akiirudia rudia na kuikariri aya isemayo: "Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa sana" (Surat Nisaai:113)

Nikajikuta machozi yakinidondoka. Yule mwanamke akanivuta karibu yake, akawa akiirudia rudia kauli yake Allah:‏ ‏‎"Na Mola wako Mlezi atakupa mpaka uridhike" (Surat Dhuha:5)

Wallahi ilikuwa ni kama vile mara yangu ya kwanza ninaisikia ayah hii, nafsi yangu ikatulia, nikamaliza ibada yangu ya Umra, nikaamua kurudi Cairo.

Kando ya siti yangu katika ndege kulikuwa na kijana wa kiume. Ndege ikafika uwanjani nikashuka.

Nikashangaa kumuona mume wa rafiki yangu akiwa katika ukumbi wa mapokezi. Nikamuuliza ni nini kilicho kuleta uwanja wa ndege? Akanijibu ya kwamba anamsubiri jamaa yake ambaye anaingia na ndege ile ile niliyo ingia nayo.

Haikupita dakika yule rafiki yake akawa ashafika. Kumbe alikuwa ni yule kijana ambaye alikuwa kando yangu katika siti.

Kisha nikaondoka pale nikiwa na baba yangu.

Haukupita muta mrefu baada ya kufika nyumbani kubadilisha mavazi yangu na kupumzika kiasi, rafiki yangu akanipigia simu. Akanieleza ya kwamba rafiki wa mume wake kapendezwa nami naanataka kuja kunichumbia.

Nilifurahi sana! nikahisi huenda Allah kanijaalia faraja baada ya tabu ya muda mrefu.

Baada ya siku kadhaa wakaja nyumbani kunichumbia kwa babayangu. Haukupita muda mrefu mpaka tukawa tushafunga ndoa.

Tukaanza maisha ya ndoa yenye upendo na furaha. Niliyapata kwa mume wangu yale yote ambayo nafsi yangu ilikuwa ikiyatamani kuyaona kwa yule atakaye kuwa mshirika wangu wamaisha, miongoni mwa upendo, huruma na wema juu ya familia yake na familia yangu.

Isipokuwa miezi ilikuwa ikipita hali ya kuwa hatuoni alama zozote za ujauzito. Nikapatwa na mfadhaiko sana juu ya suala hili, khususani ukichukulia ya kwamba muda huu nilikuwa nishafikisha umri wa miaka thelathini na sita.

Nikamtaka mume wangu tuelekee hospitali nikapime, nikikhofia huenda fursa yangu ya kupata watoto ikawa ndio ishapita!

Tukaelekea kwa daktari anayehusiana na magonjwa ya wanawake nikapata vipimo.

Baada ya kuanza kupata majibu ya kipimo cha kwanza kabisa, daktari akasema: Hakuna haja ya kuendelea na vipimo, hongera dada unaujauzito!

Tulipatwa na furaha isiyokuwa na kifani. Ujauzito ukaendelea kukua salama, ingawa nilikuwa nikipata shida kutokana na ukubwa wa tumbo, kila nilipo mweleza daktari juu ya tatizo hilo aliniambia nisiwe na khofu kwani hali hii ni kutokana na kuchelewa kwangu kupata ujauzito mpaka nimefikia umri wa miaka 36.

Sikutaka kupata vipimo ili kujua ujauzito wangu ni wa mtoto wa aina gani, kwani mtoto wa aina yoyote yule niliye andikiwa ni kheri kwangu.

Ukafika wakati wa kusubiri kujifungua na nikajifungua salama. Baada ya kuzindukana, daktari akanijia hali ya kuwa ni mwenye kutabasamu.

Akaniuliza: ulikuwa ukitamani kupata mtoto wa aina gani?

Nikamjibu: Mie nilitamani Allah aniruzuku mtoto wala si jali aina ya mtoto.

Akaniambia: waonaje nikikwambia umejaaliwa kupata Hasani, Husaini na Fatuma?!

Sikufahamu lolote nikamuuliza: wakusudia nini?

Nikashangazwa pindi alipo nieleza hali ya kuwa akinituliza, Mwenyezi Mungu mtukufu kanipatia neema ya watoto watatu! Kana kwamba Allah alijaalia wale watoto nilio tarajia kuwapata ndani ya umri wangu wote niwapate kwa mara moja rehema kutoka Kwake!

Nikadondokwa na machozi ya furaha.



Copied from "Mimi ni Muislam" ndani ya Facebook

0 comments