Friday, December 16, 2011

UDSM bado hakujatengamaa,

Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha UDSM (Daruso), imesema haijaridhishwa na hatua ya kufukuzwa wenzao 43 hivyo inajipanga kuwatetea wenzao hao kwa nguvu zote.

Juzi uongozi wa UDSM ulitangaza kuwafukuza wanafunzi 43 na kuendelea kufuatilia nyendo za wengine tisa, baada ya kubainika kuwa walihusika katika matukio mbalimbali ya vurugu na uhalifu chuoni hapo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani chuoni hapo tangu mwanzo wa juma hili.

"Adhabu waliyopewa wenzetu ni kubwa kuliko makosa wanayotuhumiwa kuyafanya. Hatuikubali, tunaipinga na tutachukua hatua kuhakikisha kwamba wanarudi chuoni kuendelea na masomo yao,” Rais wa Daruso. Simon Kilawa alisema jana.

Alieleza kuwa hatua ya kwanza watakayoichukua ni kuzungumza na uongozi wa chuo kuhusu adhabu hiyo na kuongeza; “Katika hili, tayari tumeshakubaliwa kwa sharti kwamba katika mazungumzo hayo kusiibuke vurugu yoyote.”

Alisema kama mazungumzo yao na uongozi hayatafikia mwafaka, watalipeleka suala hilo katika Bunge la wanafunzi ambalo ndio lenye maamuzi ya mwisho.

“Kwa sasa siwezi kusema nini kitakachoamuliwa na Bunge hili na mpaka sasa, hatuwezi kuchukua hatua zozote kwa kuwa bado hatujazungumza na uongozi (utawala) na kujua nini hatma ya wenzetu,” alisema Kilawa.

Kwa mujibu wa Kilawa, Daruso iliuomba uongozi wa chuo kuwaruhusu wanafunzi 35 waliosimamishwa masomo kutokana na kuwa na kesi mahakamani waendelee na masomo, lakini wameshangaa hatua zilizochukuliwa za kuwafukuza wakati walikubaliwa kuendelea na masomo.

Jumatatu wiki hii wanafunzi hao walifanya mgomo wakidai taarifa za kwa nini pesa zao zinachelewa wakati Bodi ya Mikopo (HESLB), ilishasema wamezileta chuoni.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao walivamia jengo la Ofisi za Utawala na kuwazuia maofisa na wafanyakazi wa chuo hicho kutoka au kuingia ndani, hadi watakapoletewa taarifa za pesa zao kutoka TCU.

Uongozi

Akizungumzia vurugu, uharibifu na uvunjifu wa amani uliofanywa na wanafunzi hao juzi, Profesa Mukandala alisema walimwagia vumbi chakula, kuwapiga wafanyakazi wa mgahawa, kuharibu majokofu na kushambulia mabasi yaliyopita eneo la chuo yakiwemo yanayobeba wanafunzi, hali iliyosababisha huduma hizo kukosekana kwa siku mbili.

Kwa mujibu wa Profesa Mukandala, matukio hayo ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoanza kutokea mwanzoni mwa Septemba mwaka huu na kwamba vurugu hizo zilianzishwa na kikundi kidogo cha wanafunzi ambao walipata wafuasi wachache na kuvuruga shughuli za chuo hicho.

Madai ya Wanafunzi

Profesa Mukandala alisema awali madai ya wanafunzi hao yalikuwa ni kuondolewa adhabu za kinidhamu walizopewa wenzao wachache kwa mujibu wa kanuni na sheria za chuo, lakini baadaye wakageukia suala la kupatiwa fedha zao za malazi na chakula kwa kipindi cha kuanzia Desemba 10 mwaka huu.

Alifafanua kuwa fedha hizo hutolewa kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza, ilikuwa Sh4.2 bilioni ambayo ilitolewa kwa wanafunzi wa Kampasi ya Mlimani na kwamba ziliingizwa katika akaunti tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Onyo kali

Profesa Mukandala alionya kuwa mwanafunzi yoyote atakayefanya tendo la kihalifu, ikiwamo kujaribu kuwatisha wenzake au kuendesha mkutano nje ya taratibu za chuo, atafukuzwa mara moja.

“Pia yanafanyika mawasiliano na Bodi ya Mikopo wa Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu ili wanafunzi waliofukuzwa wasipate tena mkopo wa Serikali wala kuruhusiwa kusoma katika chuo chochote cha umma,” alisema Mukandala.


Mwananchi

0 comments