Wednesday, December 28, 2011

Wanafunzi 15 St. John’s wasimamishwa masomo

na Danson Kaijage, Dodoma

UONGOZI wa Chuo Kikuu cha St. John’s mkoani hapa umewasimamisha masomo wanafunzi wake 15 kwa muda usiojulikana.

Wanafunzi hao wamesimamishwa masomo baada ya kugundulika kuwa walikuwa vinara wa mgomo chuo hapo. Taarifa ilitotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari wa chuo hicho, Karimu Meshack, ilieleza kuwa wanafunzi hao wamesimamishwa baada ya kugundulika kuwa wao ndio chanzo cha matatizo na kuanzishwa kwa mgomo chuoni hapo.

Aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Albert Mganga, Ayoub Benjamin, Eric Mkunda, Frank Nicodems, Goodluck Gadway, John Komba na Kapinga Wilson.

Wengine ni Leba Camus, Masatu Siajali, Mbogo Lyoba, Milawi Stephen, Mohammed Shambi, Mwaipasi Brown, Mwinyi Ally na Pasquina Ferdenand.

Meshack alisema wanafunzi waliosimamishwa ni wa shahada mwaka wa pili na kuongeza kuwa waliwapata kwa kutumia picha na wengine walikuwa wanabishana nao uso kwa uso.

“Tuna ushahidi wote wa wanafunzi hao kwa sababu wengi tuliwapiga picha na wengine walikuwa wanatushambulia kwa maneno uso kwa uso,” alisema.

Aidha, alisema chuo kinafunguliwa Januari 2 mwakani, hivyo wanafunzi wanatakiwa kuanza kuripoti na kuanza kujisajili Januari 3 mwakani.

Alisema usajili huo kwa wanafunzi utafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani hapa na mwanafunzi yeyote ambaye hajajisajili hataruhusiwa kuingia darasani.

Aliongeza kuwa wanafunzi hao pia wanatakiwa wawe wamemaliza madeni yote wanayodaiwa na chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuwasilisha risiti ya malipo.

Hivi karibuni mgomo ulitokea chuoni hapo na kusababisha chuo hicho kufungwa hadi Januari 2, mwakani.

0 comments