Monday, January 9, 2012

Bingwa netball mapinduzi kupata mil1

Fatma Said, Zanzibar

BINGWA wa mashindano ya netiboli ya Kombe la Mapinduzi anatarajiwa kupewa kombe na dola za Marekani 750 (zaidi ya Sh milioni moja za Tanzania).

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati hiyo ya Kombe hilo, Khamis Said Abdallah wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusiana na mgawo wa zawadi kwa washindi wa mashindano hayo.

Alisema wanatarajia kutoa zawadi kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa tatu na kwamba mshindi wa pili ni dola 500 wakati mshindi wa tatu ataondoka na kifuta jasho cha dola 250.

Alisema Kamati yake ilijipanga vizuri kuhusu suala la zawadi na walitarajia kutoa zaidi ya kima hicho cha fedha, lakini kutokana na sababu zisizoweza kuepukika wameshindwa kupata kiwango walichotaka kukitoa.

“Tulitarajia kutoa zaidi ya kiwango hicho cha fedha lakini tumeshindwa kutokana na sababu zisizoweza kuepukika," alisema.

Mashindano hayo ya netiboli yanashirikisha nchi sita zikiwemo Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Msumbiji na wenyeji Tanzania.

Tayari wenyeji Tanzania kwa upande wa wanawake wamepoteza mchezo mmoja waliocheza na Uganda ambapo walifungwa mabao 38-33 wakati kaka zao walitoka kidedea kwa ushindi wa mabao 41-36 dhidi ya Uganda.

0 comments