Saturday, September 24, 2011

Hii ndio Bakwata yetu, na adhari ya nusu hijab

Katika hatua nyingine 'Vazi la hijab' jana lilivunja Mkutano wa Bakwata na waandishi wa habari baada ya baadhi ya viongozi wa Baraza hilo Kuu la Waislamu, kushindwa kueleza maana yake.

Mkutano huo uliitishwa na Katibu wa Bakwata Wilaya Igunga, Maulid Athman Mussa ambaye alitoa tamko la kukilalamikia Chadema kwamba kiliudhalilisha uislamu katika sakata baina ya chama hicho na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.

Kuvunjika kwa mkutano huo kulitokana na maswali yaliyoulizwa kwamba vazi la hijabu linalodaiwa kudhalilisha dini hiyo inabidi liweje, hivyo viongozi hao kupandwa na jazba.

Maswali hayo yalionekana kuwachanganya na kuwapandisha jazba viongozi hao, lakini wakijitahidi kutoa ufafanuzi ingawa wao wenyewe walionekana kupishana kauli.

Shehe wa wilaya, Ally Rage alisema, hijabu inanatakiwa isitiri mwili wote wa mwanamke wa kiislamu na kuacha tu sehemu ya uso wake ndio ionekane.

Ufafanuzi huo ulionekana kushahibiana na wa mwanamke mmoja wa Kiislamu aliyekuwepo ndani ya mkutano huo, Amina Billal aliyekuwa amevaa Hijabu aliyesema ni lazima lifunike miguu na mikono.

“Hijabu ni vazi la mwanamke wa Kiislamu linalositiri mwili ambalo akivaa nguo yenye mikono mirefu ni lazima liwe refu hadi chini,” alisema Amina na kuwaonyesha wanahabari vazi lake lilikuwa limefunika mikono na miguu.

Kutokana na maelezo hayo, waandishi wa habari waliwataka viongozi hao watazame picha za tukio la Chadema na Kimario katika gazeti moja walilokuwa nalo meza kuu (sio Mwananchi) na waeleze kama DC alivaa hijabu au mtandio.

Hata hivyo, katika kujibu maswali hayo, kiongozi mmoja alitumia aya za kitabu kitakatifu cha Quaran akisema Hijabu lazima lifunike nywele kwa vile ni haramu mwanamke wa Kiislamu kuonekana nywele zake. Majibu hayo bado yalionekana kujichanga zaidi na kushindwa kufafanua kama mkuu huyo wa wilaya alikuwa amevaa jijabu au mtandio hali iliyomsukuma Imamu wa msikiti huo, Swalehe Hamisi kufafanua zaidi.

Imamu alisema vazi la hijabu liko katika aina tatu moja likiwa ni lile lililokuwa likivaliwa na wake za mtume Mohamed (s.a.w) ambalo lilikuwa likifunika maeneo yote ya mwili bila kuacha sehemu moja ya mwili inayoonekana.

“Vazi la pili la mwanamke wa Kiislamu ni lile lilokuwa likivaliwa na wafanyakazi kwa maana ya wakulima ambalo lilikuwa likimsitiri mwanamke mwili wote isipokuwa sehemu ya usoni tu,”alisema.

Alifafanua hijabu ya tatu, Imamu huyo alisema ni vazi ambalo linamfanya mwanamke asiwe amejisetiri mwili wote na kwamba vazi hilo linamruhusu mwanamke huyo kusogelewa tu na ndugu wa damu na si mtu mwingine.

“Hawa Chadema wao walienda kumwondolea hijabu mwanamke wa Kiislamu ambaye hawajazaliwa naye tumbo moja na sio ndugu zake kabisa… hawakupaswa kumsogelea kabisa DC,” alisema Imamu huyo.

Pamoja na ufafanuzi huo, waandishi wa habari waliendelea kuwabana viongozi hao watoe ufafanuzi wakiegemea katika kitabu cha Qur-an kwamba kinaeleza nini kuhusu hijab jambo ambalo liliwaudhi.



mwananchi.co.tz

0 comments