TIMU ya Taifa ya netiboli ya Tanzania ‘Taifa Queens’ jana angalau iliwatoa kimasomaso Watanzania baada ya kutwaa medali ya fedha katika mashindano ya All Africa Games yanayoendelea jijini Maputo, Msumbiji.
Mkuu wa msafara wa timu hiyo, Henry Lihaya alisema jana kuwa timu hiyo ilitwaa medali hiyo baada ya kumaliza mashindano hayo ikiwa nyuma ya Uganda ‘She Cranes’, iliyotwaa medali ya dhahabu.
Taifa Queens ilitwaa medali hiyo baada ya ushindi wa jana wa mabao 43-35 dhidi ya Botswana. “Ni medali ya kwanza kwa Tanzania tangu mashindano haya yaanze, vijana walijitahidi sana kucheza kwa nguvu maana haukuja kirahisi,” alisema Lihaya.
Taifa Queens imemaliza mashindano hayo yaliyoshirikisha timu tisa upande wa netiboli baada ya kufikisha pointi 12 sawa na Zambia iliyotwaa medali ya shaba, lakini Taifa Queens ilikuwa na mabao mengi ya kufunga.
Taifa Queen imecheza michezo nane, imeshinda sita na kupoteza miwili.
Alieleza kuwa upande wa riadha mambo yalikuwa magumu kwani Dickson Marwa alimaliza nafasi ya sita katika Nusu Marathon, huku Fabian Joseph akijitoa.
Mwaka 2007 katika mashindano kama hayo yaliyofanyika Algiers, Algeria, Tanzania ilipata medali moja ya fedha iliyonyakuliwa na Martine Sulle katika mbio za Nusu Marathon.
Habarileo.co.tz
 



 
 
 
0 comments