BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limeelezea kushangazwa kwake kutokana na kutojitokeza kwa wadau kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa Chama cha Judo Tanzania (JATA).
Kutokana na tatizo hilo, Baraza kwa kushirikiana na JATA, wameamua kuanza upya uhamasishaji kwa wadau hao kuchukua fomu ambazo zinatolewa BMT.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa BMT, Henry Lihaya, alisema hakuna hata mdau moja aliyejitokeza, hivyo wamelazimika kuingilia kati ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa muda utakaopangwa.
Lihaya alisema, hawajui sababu inayowafanya wadau hao wasijitokeze kuchukua fomu, wakati taarifa za zoezi hilo zilitolewa muda mrefu.
“Hatuwezi kusema uchaguzi utafanyika lini, hadi tutakapoona uhamasishaji umepokelewa na watu wamejitokeza kuchukua fomu, hapo tunaweza kupanga tarehe ya uchaguzi” alisema Lihaya.
Alisisitiza kuwa, uchaguzi ni lazima ufanyike haraka kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, ambako aliwaomba wapenda mchezo huo wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu.
“Hatutaki kuona viongozi wale wale wanaongoza, wapo watu wengine wenye uwezo mkubwa wa kukiongoza chama, wajitokeze hawa,” alisema Lihaya.
Awali uchaguzi huo ulikuwa ufanyike Septemba 24, lakini BMT iliusogeza mbele kutokana wagombea kutojitokeza.
Freemedia.co.tz/daima
0 comments