MCHAKATO wa kuandikwa kwa Katiba mpya umeendelea kupamba moto miongoni mwa makundi ya wananchi na sasa wanazuoni wa baadhi ya vyuo vikuu nchini wanataka katiba ijayo ivunje Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wakidai kuwa hauna faida.
Mbali na Muungano, pia wasomi hao wametaka Katiba mpya iweke kipengele cha kuruhusu rais kushitakiwa mahakamani kwa kosa atakalotenda akiwa madarakani ama baada ya kuondoka.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Mwanza na wanafunzi wa vyuo vikuu, wakati walipokuwa wakichangia mada kwenye mdahalo wa Katiba, ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT).
Katika mdahalo huo ambao watoa mada wakuu walikuwa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sheria, Prof. Chris Maina na Makamu Mkuu wa SAUT, Dk. Charles Kitima, ilielezwa kwamba katiba ya sasa imekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa wananchi.
Kwamba Katiba ya sasa inatengeneza viongozi wasiofaa sambamba na kukinzana na ile Katiba ya Zanzibar, hali inayohatarisha uhai wa Muungano wa nchini hizo mbili.
Baadhi ya wachangia mada katika mdahalo huo, Wanzagi Warioba na Jimy Luhende, walisema Katiba ya sasa imepoteza uhalali wa kuiongoza nchi. Na kuongeza kuwa endapo Muungano utaendelea, basi katiba mpya lazima itambue uwepo wa nchi tatu. yaani Serikali ya Tanganyika, Zanzibar na ile ya Muungano.
Awali, akiwasilisha mada yake, Prof. Maina, alisema kuna dosari katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwamba wakati ukiundwa mwaka 1964 yalipitishwa makubaliano 11 tu, lakini baada muasisi wa upande fulani wa Muungano kufariki dunia, hivi sasa mambo hayo yameongezwa na kufikia 22.
Alisema upo umuhimu wa kuwepo kwa mjadala wa wazi kwa ajili ya kujadili uhalali wa Muungano huo, kwani hata baadhi ya sehemu za Katiba ya sasa ya Jamhuri inapingana na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
"Kwa mfano, Ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar, inasema sheria yoyote ikipitishwa na Serikali ya Muungano haitatumika Zanzibar hadi Baraza la Wawakilishi liipitie na kuipitisha pia, katiba iliyopo sasa inawanyima Watanzania kumiliki rasilimali zao tofauti na ilivyo kwa mataifa mengine Afrika,” alisema.
Kwa upande wake, Dk. Kitima, aliibeza vikali Katiba ya sasa akisema Tanzania ya leo yenye miaka 50 ya Uhuru, haitofautiani na serikali ya kikoloni ya Waingereza wakati huo ikiitwa Tanganyika na kusisitiza kuwa Tanzania inahitajika Katiba mpya ili kumaliza matatizo yanayolikumba taifa na wananchi wake.
freemedia.co.tz/daima
0 comments