Wednesday, October 5, 2011

BMZ kuimarisha vilabu vya michezo

KATIBU Mtendaji Baraza la Michezo Zanzibar (BMZ ), Hassan Hairalla Tawakal amesema wanakusudia kuviimarisha klabu za michezo kwa kuzipatia ruzuku na vifaa vya michezo ili ziweze kuendesha shughuli zao vizuri.

Akiwasilisha ripoti fupi inayohusiana na vyama vya michezo mbele ya Kamati ya Mifugo, Uwezeshaji Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi, Katibu huyo alisema vyama 30 vya michezo mbalimbali vyenye usajili vinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa fedha na vifaa vya michezo na ruzuku.

Alisema utekelezaji wa suala hilo umekwisha anza na baadhi ya vyama vya michezo vimeshafaidika na utekelezaji wa mpango huo.

Katibu huyo alisema katika hatuwa ya kuimarisha sekta ya michezo nchini wanakusudia kuwapatia mafunzo wakufunzi na wachezaji wote ili kukuza kiwango cha michezo nchini.

Kutokana na kuwepo upungufu wa vifaa vya michezo na ruzuku Katibu amevitaka vyama vya michezo viwe vibunifu kwa kutafuta njia mbadala ya kutafuta fedha ambazo zitawasaidia kuendesha shughuli za michezo yao na vyama vyao.

Alivishauri vyama hivyo vya michezo kwa kusema kutokana na uhaba wa fedha unaovikumba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa kipato kidogo kilichopo kinatumika vizuri na kurejesha marejesho kama kawaida ya matumizi ya fedha.

Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto hiyo iliyopo kumekuwa na maendeleo katika sekta ya michezo, ambapo hadi leo vyama hivyo vipo na vinaendesha shughuli zao za michezo.



Habarileo.co.tz

0 comments