CHAMA cha Baiskeli Zanzibar (CHABAZA) kimeanza kuwaandaa wachezaji wake kwa ajili ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kulipwa, imefahamika.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu Mkuu wa Chabaza, Nassoro Ally Nassoro, alisema kwamba wa wameamua kujikita kwenye mashindano ya kulipwa kutokana na kuvunjwa moyo na serikali katika baadhi ya mashindano ya kimataifa.
Nassoro alitolea mfano wa maandalizi ya mashindano ya All Africa Games yaliyomalizika mwishoni mwa mwezi Julai, huko Maputo, Msumbiji kwamba kulikuwa na upendeleo wa kupeleka michezo ambayo imezoeleka na kuwaacha wao waliofanya maandalizi ya muda mrefu.
Alisema walitumia gharama nyingi kuwaweka kambini wachezaji wao kwa kipindi kirefu na mwisho wake ilionekana kwamba walichokifanya hakikuwa na maana.
Aidha, Nassoro alisema ili kufanikisha ushiriki wa mashindano ya kulipwa watashirikiana na mchezaji wao, Juma Lukondya ambaye mara nyingi hushiriki mashindano ya kimataifa.
Nassoro alisema mara nyingi Chabaza imekuwa ikimzuia Lukondya kushiriki mashindano ya kimataifa, wakidhani kwamba wadau ikiwemo serikali wataonyesha kujali lakini matokeo yake hawawapi ushirikiano.
tanzania daima
0 comments