Tuesday, October 4, 2011

CHADEMA wafanya vurugu

WAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Wilaya ya Igunga na Moshi Vijijini, wamefanya vurugu ikiwemo kuteketeza gari la diwani kwa moto, wakipinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika juzi.

Mjini Igunga, hali ya amani jana ilichafuka baada ya kundi la vijana wanaodaiwa kuwa ni wa Chadema kuanza vurugu za kupita wakiimba katika mitaa mbalimbali mjini humu wakidai matokeo ya ubunge yatangazwe haraka.

Saa moja asubuhi, vijana hao wakiongozwa na gari la matangazo la Chadema walipita katika barabara kuu ya Igunga wakitangaziwa kuwa chama hicho kimeshinda.

Wakati vijana hao wakifanya vurugu hizo na kusababisha huduma zote za jamii kufungwa katika mji huo, tayari baadhi ya viongozi wao akiwemo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Godbless Lema wa Arusha Mjini walikuwa wameshatoa matamko ya kukubali kushindwa.

Pamoja na viongozi wa Chadema kuwa tayari wamekubali kushindwa, gazeti hili lilishuhudia vijana hao wa Chadema wengi wakiwa wageni katika Hoteli ya Peak walipokuwa viongozi wa CCM, wakirusha mawe na kupasua kioo cha moja ya magari ya chama hicho na kusababisha vijana wa CCM kutoka nje kuwakabili.

Gazeti hili pia lilishuhudia vijana wengine wa Chadema wakijikusanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga wakidai matokeo ya uchaguzi huo kwa mawe na kuanza kuchoma moto majani makavu yanayozunguka ofisi hiyo, hali iliyosababisha Polisi kuingilia kati kwa kuwatawanya kwa maji ya kuwasha na mabomu ya machozi.

Jumla ya mabomu yaliyopigwa katika eneo hilo ni takribani saba huku idadi kubwa ya wananchi wakikamatwa kwa kusababisha vurugu hizo.

Hata hivyo, wakati hali hiyo ikiendelea, Chadema waliitisha mkutano walioita wa dharura saa sita mchana wakiwatangazia wafuasi wao kuwa wameshinda ila matokeo yanachelewa kwa madai kuwa mgombea wa CCM, Dk. Dalaly Kafumu alikuwa akikataa kusaini.

Kwa kuwa Chadema waliitisha mkutano bila ruhusa tena katikati ya vurugu, Polisi wa Kutuliza Ghasia walilazimika kwenda katika mkutano huo na kuuvunja kwa kurusha tena mabomu ya machozi eneo hilo.

Baadhi ya waandishi walioenda katika mkutano wa Chadema waliambulia kuwindwa kwa madai ya kupotosha habari, hali iliyowalazimu kuchukua tahadhari zaidi huku baadhi yao wakipoteza fahamu kutokana na mabomu yaliyokuwa yakilipuliwa na Polisi.

Juzi usiku wakati kura zikihesabiwa na vyama kujumlisha kura kutoka kwa mawakala wao, vijana wa Chadema waliandamana wakiimba kwamba wameshinda.

Wengi walikwenda katika ofisi za Halmashauri na kuizunguka huku wakiimba kulinda matokeo yao, lakini kwa jinsi muda ulivyokuwa ukienda mbele sauti zao zilipungua na baadaye akatoweka mpaka asubuhi waliporudi wakihamasishwa na gari lao la matangazo.

Polisi hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa kuwa karibu viongozi wote walikuwa katika operesheni ya kulinda amani ya Igunga mara baada ya mgombea wa CCM, Dk. Kafumu kutangazwa mshindi.

Huko Moshi Vijijini, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Chadema katika Kata ya Uru Kaskazini wanadaiwa kulichoma gari la diwani wa kata hiyo kupinga matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Uru Mrawi Wilaya ya Moshi Vijijini.

Kabla ya kulichoma gari hilo lenye namba T 171 AFX aina ya Toyota Hilux, wafuasi hao walilisukuma na kulipindua huku pia wakimjeruhi kichwani Diwani huyo, Evarist Mumburi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema vurugu hizo zilitokea juzi saa 11.40 jioni kijijini humo na hasara iliyopatikana haijajulikana.

Kamanda alisema tukio hilo lilitokana na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji hicho ambapo Proti Mauki (37) wa CCM alimshinda kwa kura 230 mgombea wa Chadema, Jonathan Kisima (32) aliyepata kura 207.

Alisema pamoja na uchaguzi kufanyika kwa amani, lakini wafuasi wa Chadema walianza vurugu baada ya Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mtendaji wa Kata hiyo, Roland Tenga kumtangaza Mauki ndiye mshindi.

“Vurugu hazikuishia kwa diwani pekee kwani wafuasi wale walimpiga pia Mwenyekiti mpya wa Kijiji na kumjeruhi juu ya jicho la kulia, lakini wote walipata matibabu na baadaye kuruhusiwa kurejea nyumbani,” alisema Kamanda Mwakyoma.

Alisema Polisi iliwakamata wakazi saba wa kijiji hicho na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika. Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Evarist Lyamuya (37), Evocati Nyaki (35), Thomas Sangawe (23), Evin Marko (25), Jonathan Kisima (32), Tea Kisima (41) na Ludovic Momboi (49).

Uchaguzi kijijini humo unatokana na aliyekuwa Mwenyekiti kupitia Chadema kujiuzulu na kuhamia CCM.



Habarileo.co.tz

0 comments