IDADI ndogo ya wasimamizi wa mtihani ya kidato cha nne ulioanza jana, imesababisha mtihani huo kuchelewa kuanza kwenye baadhi ya vituo nchini.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam, msimamizi mkuu wa mtihani katika shule ya wasichana ya Zanaki iliyoko jijini Dar es Salaam, Mwalimu Barnabas Sabiye, alisema idadi hiyo ndogo ya wasimamizi ilisababisha mtihani huo katika kituo chake kuanza saa 09:30 asubuhi badala ya saa mbili.
“Kituo changu kilipangiwa wasimamizi 10 lakini wanaohitajika ni 19, kwa hiyo tuna upungufu mkubwa,” alisema Sabiye.
Hata hivyo Tanzania Daima haikuishia hapo; ilifika katika Shule ya Wasichana Kisutu ambako hali ilikuwa ileile ya kuchelewa kuanza kwa mtihani huo.
Mmoja wa wanafunzi wa kidato cha nne katika chule hiyo, Caltas Faustine, aliliambia Tanzania Daima kuwa hakuna sababu yoyote ya msingi iliyochelewesha kuanza kwa mitihani hiyo.
Wanafunzi takribani 480,079 walianza mtihani wa kidato cha nne jana ambapo wanafunzi wa shule ni 349,578 kati ya hao wavulana ni 199,117 na wasichana ni 150,461. Wanafunzi wa kujitegemea ni 101,005, kati yao wavulana ni 49,541 na wasichana 51,464.
Wanafunzi wa QT ni 29,496 na kati yao wavulana 11,005 na wasichana ni 18,040.
Tanzania daima
0 comments