Shinyanga
MVUA kubwa zilizonyesha kwa muda wa saa tano mfululizo, juzi zimewajeruhi watu wawili huku zikiacha kaya 40 bila makazi katika Kata ya Chibe, wilayani Shinyanga.
Maafa hayo yametokea siku chache baada ya mvua iliyoambatana na kimbunga kuezua mapaa ya nyumba 104 kati ya hizo, 29 zikiezuliwa kabisa katika Kata ya Mbagala, Temeke, Dar es Salaam.
Maafa hayo ambayo tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imekwishaonya katika utabiri wake wa mwelekeo wa mvua za vuli, juzi yalibisha hodi Shinyanga baada ya mvua kubwa kunyesha kuanzia saa 12:30 jioni hadi saa 5:00 usiku.
Mbali na kuharibu makazi hayo, mvua hizo pia ziliezua makanisa matatu na zahanati moja ya kata hiyo ambayo ilikuwa katika hatua ya ujenzi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani alisema anafuatilia maafa hayo kwa lengo la kuzuia yasizidi kutokea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Amina Masenza alisema kwamba atazungumzia suala atakapofika eneo hilo baada ya kumaliza jukumu la kuhakikisha hali ya amani na usalama vinatawala katika uchaguzi mdogo wa diwani katika Kata ya Masekelo.
“Nitakwenda Chibe baadaye kwani wakazi wa Kata ya Msekelo wananipigia simu wakilalamika kuwa wanatishiwa amani na watu, hivyo nashughulikia suala hili kwanza ndipo niende huko baadaye,” alisema Masenza.
Akizungumza kwa simu Diwani wa Chibe, Mahona Kamege (CCM) ambaye pia ni mmoja wa waathirika wa mvua hizo alisema licha ya kukosa mahala pa kuishi, wakazi wake hawana chakula baada ya mazao yao kusombwa na maji na mengine kuharibiwa huku baadhi ya mifugo ambayo idadi yake bado haijajulikana ikipotea.
Alisema watoto ambao kaya zao zimeathiriwa na mvua hizo wapo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga wakipatiwa matibabu.
“Tunaomba tupatiwe sehemu ya kujihifadhi kwa muda huu ambao tunafanya jitihada za kujenga nyumba nyingine ikiwa ni pamoja na chakula, kwani tulitaka kujihifadhi katika Shule yetu ya Msingi Mwamapalala lakini nayo haipo katika hali nzuri na vyoo vyake vimeezuliwa,” alisema Diwani huyo.
Hivi karibuni, TMA ilitoa utabiri kuhusu mwelekeo wa mvua za vuli, ambao pamoja na mambo mengine unaonyesha kuwa baadhi ya maeneo nchini yatakayopata mvua juu ya wastani yatakumbwa na maafa wakati yale yatakayopata chini ya wastani yatakabiliwa na njaa.
Katika utabiri huo, TMA ilivitaka vitengo vya maafa kujiandaa kukabiliana na athari zitakazotokana na mvua hizo huku pia ikizitaka mamlaka za miji kuchukua tahadhari ya magonjwa ya milipuko.
TMA katika utabiri huo ilisema mvua hizo zingeanza kunyesha wiki ya pili ya Septemba na kutarajiwa kuendelea hadi Desemba, mwaka huu.
Mwananchi.co.tz
0 comments