MKUU wa Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, Halima Dendego, amezuia mpango wa Kamati ya Shule ya Msingi Dumila ya kutaka kubadilisha matumizi ya Kiwanja cha Mpira wa miguu cha shule ili kujengwa maduka ya biashara kwa kisingizio cha udogo wa uwanja huo.
Dendego alilazimika kuingilia kati na kuzuia mpango huo wa kubadilisha matumizi hayo, baada ya kupokea malalamiko ya wakazi wa Kijiji hicho kilichopo Kata ya Magole kuwa uwanja wa shule umegawanywa vipande vya kujenga maduka.
Mkazi wa Kijiji cha Dumila Wilayani humo, Somoleni Abeid alifichua mpango huo mbele ya Mkuu wa Wilaya aliyeongozana na Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera kuwa kisingizio kilichotumika ni baada ya uwanja huo kumegwa na barabara inayojengwa ya Magole- Kilosa kwa kiwango cha lami.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya hapa kuna tatizo kubwa la kiwanja cha shule, viongozi wa kijiji pamoja na walimu wameamua kiwanja cha shule kigawanywe kujenga fremu za maduka na mchakato umeshafanyika,” alisema na kuongeza.
“Hapa ni muda wowote watu wanagawiwa wajenge maduka sisi wananchi hatuliafiki, eneo libakie wazi ili watoto wetu wapate sehemu ya kucheza michezo, tunakuomba uingilie kati,” alisema Mkazi huyo.
Akijibu hoja hiyo, Mkuu wa Wilaya, aliamua kusitisha mpango huo na kuwataka viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Dumila na Kamati ya Shule hiyo kutobadilisha matumizi ya kiwanja hicho cha shule hata kama ukubwa wake umepungua kutokana na kumegwa sehemu ya Barabara.
“Hakuna sababu yoyote ya kubadilisha matumizi ya uwanja huu wa shule, hata kama hautoshi kwa mchezo wa mpira wa miguu, utaweza kutumika kwa netiboli na michezo mingine ikiwa na matumizi ya mikutano ya shunghuli za kitaifa,” alisema mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Dumila, Doglas Mwingumila, alikiri kuwa Kamati hiyo ilipanga kubadili matumizi ya uwanja huo baada ya kuona umemegwa na barabara.
Alisema kamati ya shule iliweka maazimio ya kufikiria kupima eneo hilo la kiwanja cha shule kwa ajili ya kuweka maduka kwa madai kuwa Barabara imepunguza eneo la ukubwa wa kiwanja hicho.
Kutokana na agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, kusitisha mpango huo, Mwenyekiti huyo wa Serikali ya Kijiji alipokea agizo hilo na kusema kuwa watatafuta eneo lingine ili wananchi wanaohitaji kujenga vibanda vya biashara waweze kujenga.
Habari leo
0 comments