ZAIDI ya wachezaji gofu wanawake chipukizi 10 nchini wameanza kunolewa na kocha Mbwana Juma kwa ajili ya kukuza vipaji vyao na kujiandaa na michuano ya Wanawake ya Uganda Open mwaka 2011.
Michuano hiyo ya kila mwaka ya Uganda Open inayoshirikisha wachezaji nyota kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati imepangwa kuanza Novemba 25 hadi 27 kwenye viwanja vya klabu ya Kitante, Kampala, Uganda.
Akizungumza na HABARILEO jijini Dar es Salaam, Rais wa Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU), Mbonile Burton alisema wamepokea mwaliko kutoka kwa Chama cha Gofu cha Wanawake Uganda (ULGU) hivi karibuni.
“Tumepata mwaliko kutoka kwa wenzetu wa Uganda kwa hiyo, tumeona ni fursa nzuri ya vijana wetu kujifua huku tukiendelea kutafuta wadhamini ili kuhakikisha tunapeleka vijana ambao wataipeperusha vema bendera ya Tanzania,” alisema.
Burton alisema kuwa chipukizi hao wakiwepo wa timu ya taifa wananolewa kwenye Viwanja vya Klabu ya Gymkhana Dar es Salaam.
“Nashukuru kocha Mbwana amekubali kusaidia vijana wetu na vijana pia wamekubali wito, tunatarajia muda wa mwezi mmoja utatosha kuwaweka kwenye hali nzuri ya kiushindani,” alisema.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunakwenda Uganda na kuzoa vikombe vyote kadri iwezekanavyo,” alisema na kuzitaka kampuni, taasisi na watu wenye mapenzi mema kuisaidia TLGU.
Burton aliwataja baadhi ya wachezaji ambao wananolewa ni mchezaji wa timu ya taifa Hawa Wanyeche, Shazi Myombe, Mwanaidi Ibrahim, Vailet Peter, Tayana William, Vicky Elias, Halima Mussa, Chiku Elias, Habiba Sanze na Mariam Hiza.
Alisema mafunzo hayo ni ya wazi kwa wachezaji wote chipukizi. Burton alisema mbali na wachezaji wa Dar es Salaam, anatumaini walio mikoani nao wanajifua ili kuhakikisha lengo lao linatimia.
Mara ya mwisho Mtanzania kunyakua taji la Uganda Open ilikuwa mwaka 2005, veterani Sophia Viggo alipofanya hivyo.
Habari leo
0 comments