Tuesday, October 25, 2011

Kenya na Tanzania kubadilishana wafungwa

WAFUNGWA wa Tanzania walioko Kenya na wale wa Kenya waliofungwa Tanzania, wametakiwa kuwa wavumilivu wakati mkataba wa kubadilishana wafungwa kwa nchi hizo mbili ukishughulikiwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule alisema Serikali imesikia kilio cha wafungwa hao na wanaendelea kukamilisha mkataba wa nchi hizo.

Bila kutaja muda maalumu wa kukamilisha mkataba huo, Katibu Mkuu huyo aliwasihi kuwa ni lazima kuweka vipengele vitakavyokuwa na manufaa kwa nchi zote.

Akizungumza na gazeti hili jana, Haule alisema mkataba huo unashughulikiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na taratibu zitakapokamilika, wafungwa hao wataruhusiwa kuendelea na vifungo vyao nchini mwao.

Kauli ya Katibu Mkuu huyo inatokana na malalamiko ya hivi karibuni ya Watanzania zaidi ya 66 waliofungwa katika Gereza la Kamiti jijini Nairobi nchini Kenya, kwamba wanateswa na kunyimwa chakula na kuiomba Serikali kufanya utaratibu wa kuwarudisha nchini ili kumalizia vifungo vyao.

Haule alisema baada ya malalamiko ya wafungwa hao yaliyotolewa mwanzoani mwaka huu na kuripotiwa na gazeti hili, walituma maofisa kwenda kuangalia tatizo hilo na kugundua baadhi ya malalamiko ilikuwa ni msukumo kwa Serikali kuwarejesha nchini kumalizia vifungo vyao.

Pia Wakenya waliofungwa katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, nao walitoa maombi ya kurudishwa nchini Kenya kumalizia vifungo vyao ili kuwa karibu na familia zao.

Wakenya hao waliofungwa miaka 30 na tayari wametumikia miaka sita jela, waliwasilisha maombi yao kupitia ndugu yao, Iscar More huku wakisihi kubadilishana na Watanzania hao.

Awali, Balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso alinukuliwa akisema kuna makubaliano baina ya nchi hizo mbili yaliyofikiwa mwaka 2005 katika Tume ya Umoja kubadilishana wafungwa, lakini hakuna nchi iliyotuma maombi kutaka wafungwa wahamishwe. Lakini Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Mwandamizi, Omary Mtiga, alisema hayo yalikuwa ni muhtasari wa kikao waliyoafikiana kuanzisha na siyo mkataba.



Habari leo

0 comments