Monday, October 17, 2011

Maaskofu wamjia juu Kikwete

MAASKOFU wa Kanisa la Christian Mission Fellowship (CMF), wamesema kitendo cha Rais Jakaya Kikwete, kuendelea kuwakumbatia watuhumiwa wa ufisadi ndani ya serikali yake kinazidi kuwaangamiza Watanzania kwa umaskini.

Mbali na lawama hizo, pia wamesema kuwa kanisa hilo litaungana na wanaharakati wa kweli na wapenda maendeleo nchini ili kuhakikisha wanaipinga serikali kulipa deni la Dowans la sh bilioni 94.

Maaskofu hao, walitoa kauli hizo jana mjini hapa wakati wa ibada maalumu ya kumsimika Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Askofu Dorlinad Mhango, iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa CMF, Dk. Mungulu Kilimba.

Kauli hiyo inakuja siku chache tangu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, isajili tuzo ya Dowans iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), ikilitaka Shirika la Ugavi wa Umeme Nchini (TANESCO), kulipa fidia hiyo kutokana na kosa la kuvunja mkataba baina yake ya kampuni ya Dowans Tanzania.

Askofu Kilimba alisema kuwa inashangaza kuona serikali inaridhia kulipa deni hilo haraka wakati haina fedha za kuendeshea shughuli mhimu za kimaendeleo za kumkomboa Mtanzania anayeishi kwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku.

Alibainisha kuwa Kanisa kamwe halitanyamazia kitendo hicho na hivyo lazima waungane na wanaharakati nchini kuhakikisha wanapinga ulipwaji wa fedha hizo licha ya ICC kutoa hukumu ya kuitaka TANESCO kulipa fidia hiyo.

“Kamwe viongozi wa dini hatuwezi kunyamaza juu ya hili, kwani tunajiuliza kuna nini hadi serikali iridhie haraka kulipwa kwa fedha hizo wakati kuna matatizo mengi ambayo yanatakiwa kutatuliwa,” alihoji askofu huyo na kuongeza:
“Watanzania wangapi wanaishi chini ya dola moja kwa siku na hawajui hatma ya maisha yao, hawana umeme, huduma za afya ni mbovu halafu inakuwaje serikali iwe tayari kulipa deni la Dowans upesi na kuacha kushughulikia matatizo mengine muhimu? Sisi kama kanisa hapa hatuwezi kunyamaza.”

Aliitaka serikali kuueleza umma wazi wazi ni wapi fedha hizo za kuilipa Dowans zinatoka na zinalipwa kwa nani ikiwa viongozi wote wa juu akiwemo Rais Jakaya Kikwete, walikiri kuwa hawawajui wamiliki wa kampuni hiyo.

“Jamani ndugu zangu lazima tujiulize kuna nini kati ya serikali na Dowans? Wazee wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi leo wanaandamana hadi kulala barabarani hawajalipwa madeni yao, lakini leo hii serikali inaharakisha kulipa deni la Dowans, hii haiwezi kukubalika kirahisi na ni haki yetu kuhoji na kuungana na wanaharakati wa kweli wapenda maendeleo kupinga malipo hayo,” alisisitiza askofu huyo.

Katika hatua nyingine, Askofu Kilimba aliwataka watumishi wa kanisa hilo kuhakikisha wanasema ukweli juu ya mambo yanayokwenda kinyume na matarajio ya nchi hasa suala la rushwa, ufisadi na viongozi wa serikali kujilimbikizia mali wakati Watanzania wengi wanakufa kwa umaskini.

“Viongozi wa dini ni lazima kuikosoa serikali bila woga kwani sisi ndiyo kazi kubwa tunayotakiwa kuifanya, sasa angalia viongozi wa serikali wanavyojichukulia mali pamoja na kuingia mikataba mibovu na kulisababishia taifa janga kubwa la umaskini na madeni. Lazima tupige kelele kwa ajili ya kufanya mabadiliko,” alisisitiza Askofu Kilimba.

Kwa upande wake, Makamu mpya wa Askofu Mkuu, Mhango, alisema kuwa kinachosababisha umaskini nchini ni Rais Kikwete kutokuwa na maamuzi kwa viongozi aliowachagua.

Askofu Mhango alisema Rais Kikwete ameshindwa kuwa na maamuzi magumu ya kuwawajibisha watendaji wazembe na wale ambao si waaminifu na badala yake amekuwa kinara wa kuwakumbatia.

“Wapo watumishi wengi ambao amewateua kushika nyadhifa mbalimbali ambao wanatuhumiwa kwa ufisadi lakini Rais amewakumbatia anashindwa kutoa maamuzi magumu kwa lengo la kunusuru nchi katika janga la umaskini uliopindukia.

“Kuna jamaa zake wengi ambao wanatuhumiwa kwa rushwa lakini amewakumbatia. Pamoja na kutoa misemo ya kujivua gamba lakini hizo ni porojo tu wakati Watanzania wakizidi kuangamia,” alisema Mhango.

Askofu Mhango alisema kwa nafasi yake, atahakikisha anazungumza na serikali kwa kuitaka ijenge viwanda vikubwa na vidogo ambavyo ni vya ndani ili kuepukana na taifa kugeuzwa dampo la kutupa takataka kutoka nje ya nchi.


Tanzania daima

0 comments