VIJANA nchini wametakiwa kupenda michezo, hasa mpira wa kikapu ambao unasaidia kujenga mwili na afya, ikiwemo pia kutoa ajira kwa kijana.
Wito huo umetolewa mjini hapa jana na Telvin Mbarama, ambaye ni mratibu wa uhamasishaji vijana kujiunga katika mchezo huo, wakati wa tamasha la kuhamasisha lililoshirikisha timu 10.
Alisema uhamasishaji kama huo utaendelea nchi nzima na tayari mikoa sita imenufaika ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Shinyanga, Dodoma, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro.
Alifafanua kuwa katika mikoa yote hiyo waliyopita, tayari kuna mwamko mkubwa wa vijana na wengi wameonyesha kuupenda mchezo huo.
Mbarama alifafanua kwamba zoezi hilo limekuwa likifanyika kila mwaka kwa udhamini wa kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola, kupitia kinywaji chake cha Sprite.
Tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Soweto jijini hapa, pia limekuwa likiibua vipaji vya wasanii wa kizazi kipya wenye uwezo wa kuimba Hip hop, ambapo kila mkoa umekuwa ukitoa mshindi mmoja atakayeshiriki tamasha la kitaifa litakalofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 23 mwaka huu, kwenye viwanja vya Leaders Club.
Tanzania daima
0 comments