Tuesday, October 11, 2011

NHC yaipa miezi miwili serikali

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa miezi miwili kwa Wizara, Taasisi za Serikali na mashirika ya umma yanayodaiwa malimbikizo ya kodi ya pango kulipa, vinginevyo, litanyang’anya ofisi zake na kutaifisha mali za wadaiwa.

Shirika hilo linazidai wizara na taasisi mbalimbali za serikali zaidi ya shilingi bilioni mbili. Aidha, shirika hilo limesema hatua ya kudai madeni hayo ya muda mrefu kwa taasisi za Serikali sio vita kati yake na wadaiwa hao, bali utaratibu unaokubalika wa kukusanya madeni yake.

Akizungumza Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Jamii cha NHC, Susan Omari alisema shirika hilo linashindwa kutekeleza mipango yake ya kuongeza makazi bora kwa wananchi kutokana na kutolipwa madeni yake kwa wakati.

“Kwa kuwa tunategemea kodi hizo kujenga nyumba nyingine za makazi, tunatoa mwezi huu wa Oktoba na Novemba, 2011 ziwe zimelipwa, la sivyo, tutafunga ofisi …,” alisema Omari.

Hatua itakayofuata baada ya kuzifunga ni kuwapa wadaiwa notisi ya siku 14 na kukabidhi jukumu la kukamata mali zao kwa madalali wa mahakama na kuziuza ili kufidia deni.

“Ingawa tunatambua kuwa mchakato wa malipo ya madeni ya Wizara, Taasisi za Serikali na mashirika ya umma unachukua muda mrefu, haimaanishi kuwa wadaiwa hao wanapaswa kuyalimbikiza.

“Kufanya hivyo kunaligharimu shirika fedha na rasilimali nyingi katika kushinikiza lilipwe na kuendeleza shughuli zake za maendeleo,” alisema.

Alisema licha ya wadaiwa hao kufahamu kuwa NHC inajiendesha kwa kutegemea vyanzo vyake na sio ruzuku kutoka serikalini, wizara mbalimbali, taasisi na mashirika ya umma zimekuwa miongoni mwa wadaiwa sugu.

“Tunazidai wizara kadhaa na taasisi zake zaidi ya shilingi bilioni mbili ambazo ni malimbikizo ya kodi ya pango la ofisi kwa miaka isiyopungua mitatu,” alisema Omari.

Alisema tofauti na mategemeo ya shirika hilo ya kuungwa mkono na wadaiwa hao ili litekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayowataka wajenge nyumba 1,500 za makazi kwa ajili ya wananchi, wamekuwa wakichelewa kulipa na hivyo kukwazwa utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, NHC itaendelea na msimamo wake wa kutobagua wadaiwa wa kuwafukuza kwenye majengo yake endapo ulipwaji wa madeni hautageuzwa kuwa kipaumbele kwa faida ya umma.

Wizara zinazodaiwa madeni hayo ni Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (Sh milioni 586); Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (Sh milioni 391.4) na Afya na Ustawi wa Jamii (Sh milioni 325.3).

Nyingine ni Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Sh milioni 266.1); Mawasiliano na Uchukuzi (Sh milioni 67.1); Ujenzi (Sh milioni 23. 8) na Fedha (Sh milioni 32.4).

Taasisi za Serikali zinazodaiwa ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Sh milioni 46.4); Tume ya Utumishi wa Umma (Sh milioni 23.3); Msajili wa Mahakama Kuu –Tanga (Sh milioni 8.1); Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (Sh milioni 42.8).

Kuhusu hatua yake ya kufunga Ofisi za Idara ya Habari (MAELEZO) zilizopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, Omari alisema wahusika baada ya kufungiwa ofisi, walipeleka maombi ya mwezi mmoja, ili wakamilishe malipo hayo.

Habari leo

0 comments