Tuesday, October 11, 2011

Tanesco wapinga Dowans

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), leo litawasilisha katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ombi la kutaka kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kuilipa Dowans Holidings.

Uamuzi wa kuilipa Dowans uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na kupata baraka za Mahakama Kuu chini ya Jaji Emilian Mushi.

Mahakama Kuu iliridhia tuzo ya ICC hivi karibuni ya malipo ya fidia ya fedha kwa Dowans ambayo inaitaka Tanesco kulipa kiasi cha Sh111 bilioni kwa kuvunja mkataba wake na kampuni hiyo. Awali, Tanesco ilikuwa ikidaiwa Sh94 bilioni lakini baada ya kukata rufaa na kushindwa deni hilo liliongezeka riba ya asilimia 7.5.

ICC iliamuru Tanesco kuilipa Dowans Holdings SA(Costa Rica) na Dowans Tanzania kutokana na kukatisha mkataba wa uzalishaji wa umeme kati ya pande hizo mbili mwaka 2008.

Mmoja wa kundi la wanasheria wa Serikali anayeshughulikia suala hilo, Dk Eve-Hawa Sinare alisema jana kuwa ombi hilo la kutaka kukata rufaa litafuatana na ombi jingine la rufaa ya kutaka kuzuia uamuzi wa malipo hayo usitekelezwe kwanza kabla ombi hilo kusikilizwa.

Dk Sinare ambaye pia ni mmoja mawakili katika kampuni ya Rex Attoneys alisema hutua itakayofuata baada ya ombi hilo ni kuomba nakala halisi za mwenendo wa kesi hiyo, hukumu na tuzo iliyotolewa kwa ajili ya kukata rufaa waliyokusudia katika Mahakama ya Rufani.

Alisema kuwa Tanesco walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu kwa sababu waliamini kuwa mahakama hiyo haikuangalia mambo muhimu na yenye utata kisheria katika kesi hiyo yenye manufaa ya umma.

mwananchi

0 comments