Wednesday, October 26, 2011

Timu ya taifa kukosa Dar open

WAKATI joto la michuano ya gofu ya Kombe la Challenge Afrika Mashariki likianza kupanda, timu ya taifa ambayo itatangazwa kesho itakosa mashindano ya taifa ya Dar es Salaam Open.

Michuano ya Kombe la Challenge inayoshirikisha nchi tano Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na wenyeji Tanzania imepangwa kuanza Novemba 7 hadi 11 kwenye Viwanja vya Klabu ya Gymkhana Arusha.

Akizungumza na HABARILEO kutoka Arusha, kocha wa timu ya taifa Mzimbabwe, Farayi Chitengwa alisema kikosi rasmi cha wachezaji 8 watakaounda timu ya Taifa kitatangazwa kesho.

“Tunatarajia kutangaza kikosi cha wachezaji 8 wa timu ya taifa Alhamisi,” alisema.

Chitengwa aliongeza kuwa vijana 12 ambao wanaongoza kwa pointi za ‘Order of Merit’ wanajifua kwenye Klabu ya Gymkhana Arusha ambao kati yao watachujwa na kubaki 8.

Mashindano ya taifa ya KCB Dar es Salaam Open yamepangwa kuanza Oktoba 29 hadi 30 kwenye Viwanja vya Klabu ya Lugalo, Dar es Salaam.

Vijana wanaojifua kuwania kuwepo kwenye timu ya taifa ni Adam Abbas, Frank Roman, Nuru Mollel, Elisante Lembris, John Leonce, John Saidi, Jimmy Mollel, Isaac Anania, Godfrey Leverian, Michael Makala na Amani Saidi aliyechukua nafasi ya Pembe Kondo ambaye amejitoa mwenyewe.

“Kutokana na mashindano kukaribia tunatarajia vijana wa timu ya taifa watabaki Arusha kwa ajili ya kambi hivyo, hawatasafiri Dar es Salaam kushiriki mashindano ya taifa ya Dar es Salaam Open.”

Hali hiyo inaonesha jinsi homa inavyozidi kupanda na mkakati ambao Tanzania inajiwekea kuhakikisha wanachukua Kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002.

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi hivi karibuni alimuonya kocha Chitengwa kwamba ushindi pekee ndio utakaookoa kibarua chake.



Habari leo

0 comments