Friday, October 28, 2011

Wanafunzi wafunga barabara, wavamia kituo cha polisi

VURUGU kubwa ziliibuka jana baada ya wanafunzi wa Shule za Msingi Mburahati na Bryceson zilizoko Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kufunga barabara na kuandamana hadi Kituo cha Polisi Kigogo baada ya mwenzao Zuhura Bashiri (8), kugongwa gari. Mwanafunzi huyo wa darasa la kwanza ambaye alijeruhiwa vibaya, alifikwa na balaa hilo majira ya mchana na kukimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.

Tukio la wanafunzi hao kufunga barabara na kuvamia kituo cha polisi, lilitokea saa 6.40 mchana muda mfupi baada ya gari aina ya Toyota Land Cruiser kumgonga mwanafunzi huyo akiwa katika eneo la shule.

Mbali na mwanafunzi huyo, gari hilo pia lilimgonga na kumuua papo hapo mtu mwingine aliyetambulika kwa jina la Musa Ramadhan (16), muuza magazeti , mkazi wa Manzese Uzuri jijini Dar es Salaam.

Baada ya kufika Kituo cha Polisi Kigogo, wanafunzi hao walipaza sauti na kuimba 'Tumechoka kuona maiti za wenzetu... tunataka haki yetu, tujengewe matuta!" Wakati wakiendelea kuimba, baadhi yao walikuwa wakipanga magogo barabarani ili kuzuia magari kupita kwenye barabara hiyo."Matuta ya namna hii ndiyo tunayotaka yawekwe," walisikika baadhi yao wakisema huku wakiendelea kufanya kazi hiyo.

Mmoja wa wanafunzi hao, Juma Athuman aliliambia gazeti hili kuwa kama serikali ingesikia kilio chao cha muda mrefu, ajali hiyo isingetokea. "Tumekuwa tukilalamikia suala hilo siku nyingi lakini hakuna majibu ya madai yetu na wenzetu wanazidi kuumia kila siku," alisema.

Wakati wanafunzi hao wakiendelea kupanga magogo hayo, polisi waliokuwa kituoni hapo waliwafuata na kuwasihi warudi shuleni kwa maelezo kwamba taratibu za kushughulikia madai yao, ziendelea.

"Tayari tumeshamkamata dereva aliyesababisha kifo hicho na kumjeruhi mwenzenu, tunawaomba sasa mrudi shuleni kuondoa usumbufu," alisema polisi mmoja wa kike ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kile alichodai si msemaji wa jeshi hilo. Polisi huyo, alisema Zuhura alipelekwa Muhimbili na kulazwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na dereva wa gari hilo aliyemtaja kwa jina la Ratifa Barigi, anashikiliwa na jeshi hilo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mburahati, Mahmoud Biwi, alisema kuwa wanafunzi hao waliamua kuandamana baada ya kuchoshwa na matukio ya ajali katika eneo hilo. Alisema katika kipindi mwaka mmoja uliopita, wanafunzi saba wamegongwa magari na kujeruhiwa vibaya, wawili kati yao walipoteza maisha.

“Wanafunzi wa shule zote wameamua kuandamana na kufunga barabara baada ya mwenzao kugongwa katika eneo hili ambalo kwa muda mrefu tumeomba tuwekewe matuta lakini hakuna kinachoendelea hadi sasa. Leo (jana) ni ajali ya saba inayomhusisha mwanafunzi wetu,' alisema. Diwani wa Kata ya Mburahati, Mwakilinga Mwakalinga alisema tatizo hilo linafahamika na tayari ameomba fedha manispaa kwa ajili ya ujenzi wa matuta.

"Tatizo linafahamika, Jumatatu tunaanza kuweka matatu ya dharura huku tukiendela kusubiri kupitishwa bajeti yetu itakayotuwezesha kujenga matuta ya kudumu," alisema Hata hivyo alisema barabara hiyo inamilikiwa na serikali kuu na mchakato mzima wa ukamilishaji wa ujenzi wake bado unasimamiwa na Wakala wa Ujenzi wa Barabara nchini (Tanroads). Hii ni mara ya pili wanafunzi kuziba barabara wakishinikiza kujengwa matatu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Julai 28, mwaka huu Polisi Mkoa wa Ilala, walilazimika kutumia gari lao kubeba wanafunzi wa Shule ya Msingi Minazi Mirefu, kuwarudisha shuleni baada ya watoto hao kuandamana wakishinikiza kujengwa matuta barabarani.

Shinikizo hilo lililenga kupuguza ajali za mara kwa mara katika eneo shule hiyo iliyopo eneo la Ukonga Banana. Maandamano hayo yalifuatia tukio la wanafunzi wawili wa shule hiyo kugongwa na gari na kukimbizwa hospitalini.
Siku chache baada ya tukio hilo, wanafunzi wa Shule ya Msingi Mzimuni Kinondoni jijini Dar es Salaam nao walifunga barabara ya Mikumi kwa takribani saa 1:35 wakiishinikiza manispaa hiyo kuweka matuta.

Hatua hiyo, ilikuja baada ya mwanafunzi mwenzao wa darasa la tatu, Godfrey Mussa kugongwa na gari karibu na eneo la geti la shule hiyo. Mbali na matukio hayo ya karibuni, Septemba 29 mwaka juzi, wanafunzi zaidi ya 200 wa Shule ya Sekondari Kibasila, jijini Dar es Salaam, walilala kwenye makutano ya Barabara ya Mandela na Chang’ombe na kuifunga kwa muda wa saa tano wakiishinikiza serikali kuweka matuta eneo la shule hiyo.

Wanafunzi hao walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na maandishi yenye ujumbe unaoitaka serikali kuweka alama za barabarani pamoja na matuta ili kutoa tahadhari kwa madereva, ambao wamekuwa wakiendesha magari kwa mwendo kasi.

mwananchi

0 comments