Sunday, November 13, 2011

Dewji: Waislam jengeni miundo mbinu

MBUNGE wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji amewasihi waumini wa dini ya Kiislamu jimboni kwake kuhakikisha ujenzi wa misikiti unakwenda bega kwa bega na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya huduma za jamii, kama wanavyofanya waumini wa dini ya Kikristo.

Dewji aliyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa Msikiti wa Rahman uliopo Kata ya Kindai mjini hapa juzi ambao unaokadiriwa kugharimu Sh milioni 55.8 hadi utakapokamilika.

Alisema kuwa miundombinu ya huduma za jamii kama vile afya, maji na elimu inanufaisha watu wengi zaidi wakati ujenzi wa misikiti unalenga kuwanufaisha waislamu tu.

“Igeni wanayofanya wenzenu Wakristo kwa kuweka huduma za kijamii. Serikali yetu ni maskini, tusiitegemee kwa kila kitu. Tuiunge mkono hasa katika kujenga huduma mbalimbali za kijamii,” Dewji alisema.

Dewji aliwahakikishia waumini hao kuwa pale watakapoanzisha huduma za kijamii, naye atakuwa radhi kuwaunga mkono mara moja.

Aidha, Mbunge huyo aliwahimiza wazazi wote kuwapeleka watoto wao shule ili si tu wapate elimu bali wapate elimu bora. Elimu ambayo itakayowafanya wasiwe tegemezi katika siku za usoni.

Katika hafla hiyo, Dewji aliahidi kutoa msaada wa mifuko 500 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo na Sh milioni moja kwa ajili ya eneo ya watoto katika eneo hilo.

Awali, mbunge huyo alitembelea miradi mbalimbali inayofanywa na Kanisa la Pentekoste mjini hapa (FPCT) na kuweka jiwe la msingi la Kituo cha Vijana ambapo aliwasifia kwa juhudi zao za kuendeleza jamii.

Aliahidi kuwapa cherehani 10, Sh milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho na kusaida mikopo kwa akinamama.


Habari Leo

0 comments