Sunday, November 13, 2011

VIONGOZI WA WAONYA, WATAKATA MWAFAKA HARAKA

MSUGUANO kati ya Serikali na Chadema sasa ni bayana kufuatia kauli mbalimbali za viongozi wa Serikali kukosoa hadharani mwenendo na utendaji wa chama hicho kikuu cha upinzania nchini.

Hatua hii imekuja wakati hali tete ya kisiasa ikiendelea kugubika Jiji la Arusha huku Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiri hadharani kuwa maandamano yanayofanywa na Chadema kwa kaulimbiu ya 'Nguvu ya umma,' yanainyima usingizi serikali.

Mbali na Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa Mulungo, amekuja juu na kudai kuwa harakati zinazoendeshwa sasa na Chadema, hazina nia njema na kwamba ni mkakati wa maksudi kutaka mkoa huo usitawalike.

Wachunguzi wa mambo ya siasa nchini wanatafsiri kauli za viongozi hao kuwa zimefungua ukurasa mpya unaodhihirisha kuwepo msuguano mkubwa na wazi kati ya Serikali na Chadema.

Kwa muda mrefu Chadema imekuwa ikilaumu mambo kadhaa ikiwemo kunyimwa vibali vya maandamano na makada wake kuswekwa rumande na kudai kwamba nyuma ya matukio hayo, kuna mkono wa Serikali.

Mwanzoni mwa wiki hii viongozi wa Chadema akiwamo, Katibu Mkuu wake, Dk Wilbroad Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu walikamatwa kwa kosa la kufanya mkusanyiko bila kibali cha polisi katika Uwanja wa NMC mjini Arusha.

Hata hivyo, hatua hiyo inaonekana kupingwa na baadhi ya viongozi wa dini, wanasiasa na wafanyabiashara mkoani Arusha kwa maelezo kwamba vurugu, vitisho na matumizi ya vyombo vya dola kamwe hayawezi kuleta suluhu ya migogoro ya kisiasa na kushauri kuwepo mazungumzo na majadiliano kati ya makundi husika.

Kauli za viongozi wa dini Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti jana, Askofu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer na Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Wilaya ya Arusha, Abbas Ramadhani Mkindi ‘Darweshi,’ kwa pamoja waliwataka viongozi wa serikali na vyama vya siasa mkoani Arusha, kuacha ubabe, vitisho na kuhasimiana badala yake waonyeshe nia ya kweli kumaliza mgogoro huo.

“Hali ni mbaya Arusha katika nyanja zote. Kisiasa kuna machafuko yanayotuathiri wote, waliomo na tusiokuwemo. Katika matatizo na machafuko haya, huwezi kunyooshea kidole mtu au chama chochote cha siasa, muhimu hivi sasa ni kufanyika majadiliano bila ubaguzi wala kudharauliana ili turejeshe amani mjini mwetu,” alishauri Askofu Laizer alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.

BOFYA HAPA KWA KUSOMA ZAIDI

0 comments