Wednesday, November 2, 2011

Mjerumani: Tanzania bado katika michezo

MKUFUNZI wa Michezo kutoka Ujerumani aliyekuwa nchini kwa miaka minne akiendesha program mbalimbali za michezo, Hans-Peter Thumm amesema hata aje kocha wa aina gani kutoka nchi iliyoendelea kisoka, kamwe Tanzania haitafanya vizuri.

Akizungumza katika hafla fupi ya kumuaga kabla ya kuondoka kurudi Ujerumani, alisema katika kipindi alichokaa Tanzania hakuna chochote kinachoweza kuwapa matumaini ya kujivunia katika medani za soka na hata michezo mingine.

"Hata walete kocha kutoka wapi, alikuja kocha kutoka Brazil mambo yale yale, kwa sasa yuko kocha kutoka nje (Jan Poulsen), lakini hakuna kitu, hakuna matumaini yoyote ya kucheza hata Kombe la Dunia, hilo halina ubishi na halipo.

"Mbali na soka, Tanzania hakuna hata matumaini ya kupata medali kwa Michezo ya Olimpiki ya London mwakani na nina sababu nitazisema," alisema Thumm aliyeitwa nchini kwa ushirikiano wa Kamati ya Olimpiki ya Ujerumani na serikali ya Tanzania kupitia Kamati ya Olimpiki, TOC.

Alisema kuwa kama Tanzania inataka kutwaa medali kwa mashindano yoyote, lazima kufanya maandalizi kwa miezi 11, lakini si wiki tatu kabla ya mashindano au kuingia kambini mwezi mmoja.

"Hilo halipo, mtaendelea kulaumiana. Huwezi kukaa mwezi mmoja kambini eti ndiyo unakwenda Olimpiki au Michezo ya Afrika, hilo msahau.

Alisema Tanzania hakuna sera ya michezo na vile vile viongozi wa serikali wanaosimamia michezo, wanatakiwa kubadilika na kutengeneza misingi ya kweli kupata wanamichezo. BMT imekuwa ikitetea kuwepo na sera ya michezo Tanzania.

Kingine alichokigusia ni Vyama na Mashirikisho ya Michezo Tanzania kuwa hayana mipango na weledi wa kusimamia michezo.

"Viongozi wanaoingia huko hawajui kwanini wameingia nina wengine hawajawahi kucheza na ndiyo maana michezo inakufa.

Jambo lingine alilosema ni serikali kuanzisha shule za michezo kwa ajili ya kuwekeza na ndiyo inaweza kuwa msingi mzuri. "Suala hapa ni la utambuzi wa vipaji, hilo ni tatizo na kuna haja ya kutambua vipaji na kuvipeleka shule," alisema.

Akizungumzia makocha na walimu wa michezo wazawa, Mjerumani huyo aliyetunga na kitabu cha Maendeleo ya Michezo Tanzania, alisema kuwa tatizo lingine la Tanzania ni makocha.

"Huwezi kuwa na makocha ambao hawakwenda shule, lazima kuwa na makocha waliosomea hasa mchezo husika, si kwamba mtu alicheza basi ndiyo sababu, utaalamu na ujuzi zaidi unahitajika kwa ajili kuzalisha mchezaji wa kweli.

"Unaitwa kocha, hujasomea hata misingi ya ukocha, utawaharibu tu wachezaji kwa kuwa huna mbinu…unasema umechezea Simba au Yanga, si kigezo, lazima elimu ya ukocha iwepo," alisema.

Akizungumzia mfumo wa michezo, alisema Tanzania imebahatika kuwa na mfumo mbovu na hata waje makocha wanaoheshimika duniani, kamwe hakutakuwa na mabadiliko kutokana na mfumo mzima.

Anasema katika miaka yake minne Tanzania anashangazwa kuona michezo mingi inafanyika Dar es Salaam na kusema vipaji viko mikoani.

"Nimekwenda Tabora, Mbeya kuna vipaji, lakini kila siku Dar es Salaam, timu Dar es Salaam hatuwezi kufika."



mwananchi

0 comments