MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesitisha safari za mabasi 14 ya kampuni za Dar Express kutoa huduma kati ya Dar es Salaam- Arusha na Arusha-Tanga kuanzia kesho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sumatra jana, mamlaka hiyo kupitia kifungu namba 15 cha Sheria ya Sumatra namba 9 ya mwaka 2001, imeiagiza Kampuni ya Dar Express kusitisha utoaji huduma kwa magari yake yote yanayotoa huduma ya usafiri kati ya Dar -Arusha na Arusha- Tanga kuanzia kesho.
"Kutokana na kuwapo kwa matukio mengi ya ajali yaliyohusisha mabasi yanayomilikiwa na kampuni hiyo kwa kipindi kisichozidi miezi 10, mamlaka inatilia mashaka sifa za madereva wa mabasi ya Kampuni ya Dar Express," inaeleza taarifa hiyo.
Pia, taarifa hiyo ilieleza kuwa imebainika Kampuni ya Dar Express imekiuka Kanuni namba 22 ya Kanuni za Ufundi na Usalama na Ubora wa Huduma kwa Magari ya Abiria za 2008.
"Kuanzia Januari 2011 hadi sasa, mabasi ya Kampuni ya Dar Express yamehusika katika matukio ya ajali maeneo mbalimbali ambayo kampuni hiyo inatoa huduma za usafirishaji abiria.
Matukio hayo ni kama lile la Januari 4, mwaka huu basi la Dar Express lilimgonga mpanda pikipiki na kusababisha kifo maeneo ya Kifaru- Mwanga, mkoani Kilimanjaro. Kwa mujibu wa taarifa za polisi chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi," ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa Septemba 22, mwaka huu, basi la Dar Express likitokea Arusha kwenda Tanga lilimgonga mtembea kwa miguu Ramadhani Hassan na kusababisha kifo eneo la Mkumbara - Mombo na Oktoba 24, basi jingine la kampuni hiyo liligonga gari jingine kwa nyuma kisha kuacha njia na kupinduka maeneo ya Kitumbi - Korogwe. Katika ajali hiyo watu tisa walijeruhiwa.
Mwananchi



0 comments