Wednesday, November 2, 2011

Ofisi za TAKUKURU zanusurika kuchomwa

OFISI za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilaya ya Mbarali imenusurika kuteketezwa kwa moto baada ya watu wasiojulikana kumwaga petroli kwa lengo la kuteketeza nyaraka zilizokuwamo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Anaclets Malindisa alithibitisha tukio hilo na kusema Polisi inashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni mfanyabiashara Happy Shayo, wa Rujewa, Mbarali na mkazi wa Igando, Makambako, Alex Nombo (20), ambaye alijeruhiwa begani na mguuni kwa risasi wakati wa jaribio hilo huku mwenzake akifanikiwa kutoroka.

Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda Malindisa alisema watu hao walifika katika ofisi hizo saa 8 usiku na kuzimwagia petroli kwa lengo la kuzichoma lakini kabla hawajafanikiwa, mlinzi aliwaona na kufyatua risasi ambayo ilimjeruhi mmoja wao.

Alisema baada ya Nombo kujeruhiwa kwa risasi, mwenzake alikimbia, na alipohojiwa alidai kuwa walifuatwa na mfanyabiashara wa kijijini kwao, Makambako, Iringa akiwataka wachome ofisi hizo na kwamba walielekezwa kilipo chumba walichotakiwa kukichoma.

Aidha, Malindisa alisema uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kubaini watu wanaohusishwa katika tukio hilo na kuwakamata waliofanikiwa kukimbia.

Kadhalika, alisema mtuhumiwa aliyejeruhiwa amehamishwa kutoka hospitali ya Misheni ya Chimala na kuhamishiwa hospitali ya rufaa Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.

Kamanda wa Takukuru wa Wilaya ya Mbarali, Ramadhani Ndwata, hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa uchunguzi bado unaendeleo. Hata hivyo, chanzo na sababu za jaribio hilo la kutaka kuchoma ofisi hizo bado havijajulikana.



Habari leo

0 comments