Saturday, November 12, 2011

Tanzania yatoka patupu gofu

TANZANIA wameshindwa kutumia vema uwanja wa nyumbani na kupoteza tena Kombe la michuano ya gofu ya Challenge Afrika Mashariki iliyomalizika Arusha jana.

Katika michuano hiyo timu ya wanaume ya Tanzania kwa mara nyingine wamekubali kombe kwenda Kenya ambao sasa wametwaa taji hilo kwa mara ya tisa tangu kuanzishwa mwaka 1999.

Kenya ambao mwaka jana walimaliza sawa na Uganda kwa pointi, kabla ya wenzao kupewa ubingwa kwa kigezo cha kuwa watetezi, wameibuka mabingwa kwa kukusanya pointi 21 katika michuano hiyo iliyoanza Jumatano.

Tanzania ambao wameshindwa kurejea historia ya mwaka 2002 walipotwaa taji hilo mara ya mwisho kwenye michuano iliyofanyika Arusha pia, wamemaliza katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 19.5.

Timu ya taifa ilikuwa ikikabana koo kwa pointi 7 na Kenya katika raundi ya kwanza, lakini walipoteza mwelekeo kuanzia raundi ya pili hivyo kushindwa kutimiza kiu ya Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ,Dioniz Malinzi aliyetaka timu hiyo ya wanaume kufuata nyayo za dada zao ambao walitwaa Kombe la Challenge Afrika Mashariki na Kati Dar es Salaam Agosti.

Kenya walionekana tangu mwanzo kuwa na uchu wa kurejesha taji hilo walilopoteza miaka miwili iliyopita kwa Uganda ambao safari hii wamemaliza katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 10, Rwanda wamekuwa wa nne pointi 5 na Burundi wameshika mkia wakiwa na pointi 4.5.

Ilikuwa timu pekee kutoka nje ambayo ilikuja Tanzania mapema kuzoea Uwanja na kushiriki michuano ya taifa ya Tanzania Open ambayo Kombe pia limekwenda Kenya.

Timu ya taifa ambayo ilikuwa chini ya kocha Farayi Chitengwa ni nahodha Frank Roman, Abbas Adam, John Leonce, John Saidi, Elisante Lembris, Nuru Mollel, Aidan Nziku na chipukizi Isaac Anania na Victor Joseph.


Habari Leo

0 comments