WATANZANIA sasa wanaweza kufaidika na elimu bora yenye viwango vya kimataifa kutokana na kuzinduliwa kwa programu kabambe za elimu Chuo Kikuu Mzumbe.
Programu hizo za shahada za uzamili za Uchumi na Fedha katika Maendeleo na ya Uchambuzi wa Sera na Maendeleo kwa asasi zisizo za kiserikali zinaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Bradford cha Uingereza.
Shahada hizo zilizinduliwa jana na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Joseph Kuzilwa katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe jijini Dar es Salaam.
Alisema chuo hicho na kile cha Bradford wanaamini kwamba programu ya Uchumi na Fedha katika Maendeleo ni muhimu kwa Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea.
“Shahada hii ni muhimu sana hasa kwa sasa ambapo dunia inashuhudia anguko la uchumi hivyo uelewa wa masuala ya fedha katika uchumi wa dunia ni muhimu sana.
“Kwa uelewa wetu, hakuna chuo chochote katika ukanda huu kinachotoa programu za elimu kama hizi zinazogusa masuala ya maendeleo na uhalisia,” alisema Profesa Kuzilwa.
Alifafanua kwamba kozi hizo zimehakikiwa na Chuo cha Bradford na kuidhinishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Awamu ya kwanza ya wanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Uchambuzi wa Sera na Maendeleo kwa asasi zisizo za kiserikali ilianza Machi mwaka huu na wanafunzi 39 watamaliza baada ya mwaka mmoja.
Awamu ya pili ya kozi hiyo yenye wanafunzi 28 na awamu ya kwanza ya Shahada ya Uzamili ya Uchumi na Fedha katika Maendeleo yenye wanafunzi 109 ilianza katikati ya mwezi uliopita.
Alisema wakati Mzumbe itadahili wanafunzi, kutoa vifaa vya kufundishia, kusoma na mwongozo wa kusoma; Bradford itachangia vyenzo za kusomea kama vile maktaba kwa njia ya mtandao, vitabu na machapisho na kuhakikisha udhibiti.
Habari Leo
0 comments