Saturday, December 3, 2011

NECTA watishia kufuta matokeo Bukoba

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), lilitishia kufuta matokeo ya darasa la saba ya Shule ya Msingi ya Kaizilege English Medium & Boarding Scholl (KEMEBOS), iliyoko manispaa ya Bukoba, Kagera, iwapo itabainika kuwa walifanya udanganyifu katika mtihani huo.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Ofisa Uhusiano wa NECTA, John Nchimbi, wakati akijibu shutuma zilizoelekezwa kuwa shule hiyo ilifanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba kwa kuwaonyesha majawabu watahiniwa wake.

“Tumesikia taarifa hizo, lakini hatujazipata rasmi, iwapo itagundulika ni kweli sheria inasema wazi ni kuifutia matokeo shule hiyo na wahusika kuwafikisha katika vyombo vya sheria na haitakuwa mara ya kwanza kufanya hivyo,” alisema Nchimbi.

Alisema kiutaratibu kila mkoa huwa wanayo kamati ya kusahihisha mitihani ambayo mwenyekiti wake ni mkuu wa mkoa (RC) na katibu wa kamati hiyo ni ofisa elimu wa mkoa (REO) na kwamba kamati hiyo inayo mamlaka ya kuunda tume kuhoji mtu yeyote inapobaini dosari katika usahihishaji, kisha baraza hupelekewa taarifa kwa maamuzi.

Nchimbi alisema suala hilo bado lina utata na kuongeza kuwa pamoja na kusubiria taarifa za mikoa yote nchini kabla ya kutoa matokeo haitawazuia na wao kufanya uchunguzi.

Habari zilizoenea mjini hapa, zinadai kuwa mchezo huo ulichezwa kati ya wasimamizi waliosimamia mtihani wa taifa, wakishirikiana na walimu wa shule hiyo.

Inadaiwa kwamba shule hiyo ambayo pia ina shule ya sekondari, imekuwa ikifanya mchezo huo kwa miaka mingi kwa nia ya kujiongezea sifa katika soko hili la ushindani wa kibiashara katika sekta ya elimu mkoani humo.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Yusto Kareju, alipohojiwa na gazeti hili, alitoa maneno ya kashfa, huku akimfokea mwandishi wa habari akisema hataki kuelezwa upuuzi.


Tanzania Daima

2 comments:

  1. Mmh, mambo ya elimu bwana! Inabidi walimu wawe wanatoa elimu bora ambayo itawafundusha na kuwaelimisha vizuri wanafunzi na kuwapata uwezo mzuri wa kujibu mitihani na kufaulu pasipo kuibia!

    ReplyDelete