Saturday, December 10, 2011

Shangwe za CHADEMA zatawala mkesha wa Uhuru

SHEREHE za mkesha wa miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja juzi, jijini Dar es Salaam ziliingia dosari baada ya askari kadhaa kutaka kuwakamata watu waliokuwa wakipiga kelele za kukishangilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kundi kubwa la watu wengi wao wakiwa vijana wa rika mbalimbali walishangilia kwa nguvu na kukitaja CHADEMA, kila mlio wa fataki ulipokuwa ukisikika, hali iliyowavutia wananchi wengine kujiunga na kundi hilo.

Kelele za kukishangilia CHADEMA zilidumu zaidi ya robo saa, kiasi cha kuonekana kuwaudhi baadhi ya viongozi wa serikali walioalikwa katika mkesha huo ambao mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Polisi wenye mbwa na wale waliokuwa wamesheheni silaha, walijaribu kulizingira kundi hilo na kulitaka kutokitaja chama hicho, lakini walikumbana na wakati mgumu baada ya kuambiwa wakamnyamazishe kwanza, Kapteni John Komba ambaye alikuwa jukwaani akitumbuiza kwa kuisifia zaidi CCM.

Hatua ya polisi hao ilisababisha kukusanyika kwa watu wengine zaidi, na kuzua zogo kubwa kutoka kwa wananchi, waliodai kuwa wamelazimika kuingiza kibwagizo cha CHADEMA kila ilipopigwa fataki moja, kutokana na kukerwa kwao na tukio la viongozi wa serikali kutaka kuzifanya sherehe hizo zionekane kuwa za Chama Cha Mapinduzi wakati ni suala la Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama.

Kutokana na mshikamano wa wananchi hao, polisi hao walilazimika kubaki kimya na kuacha shangwe za CHADEMA ziendelee hadi ratiba ya kuondoka kwa mgeni rasmi na wageni wengine ilipowadia.

Hata hivyo, ulipuaji huo wa fataki uliingia dosari kubwa katika viwanja vya Mbagala Zakheim jijini Dar es Salaam, baada ya watu watatu kuzimia na mmoja akiwa katika hali mbaya baada ya kusikika kwa milio hiyo.


Soma zaidi katika Tanzania Daima

0 comments